Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiinua juu na kunyesha Kitabu cha Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa rasimu hiyo uliofanyika leo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, (kushoto) ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, Joseph Sinde Warioba.

Meza kuu ikiwa na baadhi ya Viongozi wakuu wa Serikali na Jukwaa la Tume ya Katiba mpya.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe (kulia) akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake katika hafla ya uzinduzi wa rasimu ya Katiba hiyo.

Baadhi ya wazee waasisi waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo leo.

Sehemu ya waandishi wa habari wakiwa bize kunakili kila kinachozungumza mahala hapo.

 Sehemu ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, waliohudhuria hafla hiyo, wakiwajibika. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
DONDOO ZA RASIMU YA KATIBA MPYA NI KAMA ZIFUATAZO:-
 1. Tume ilifanya mikutano 1,942 ambayo ilihudhuriwa na wananchi wapatao 1,365,337 ambao kati ya hao wananchi 333,537 walitoa maoni ama kwa mazungumzo ya ana kwa ana au kwa maandishi.
 2. IBARA ZINAZOPENDEKEZWA KWENYE RASIMU YA KATIBA
 • MISINGI MIKUU YA TAIFA

Tume imependekeza Katiba iwe na Misingi Mikuu saba ya Taifa;yaani; Uhuru, Haki, Udugu, Usawa, Umoja, Amani na Mshikamano.

 • TUNU ZA TAIFA

Tume imependekeza Tunu zifuatazo zitajwe ndani ya Katiba. Tunu hizo ni;- Utu, Uzalendo, Uadilifu, Umoja, Uwazi, Uwajibikaji na Lugha yetu ya taifa ya Kiswahili.

 • MALENGO YA TAIFA

Tume imependekeza malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa mpangilio wa kuonesha malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kimazingira na sera ya mambo ya nje. Malengo hayo yameingizwa kwenye Rasimu ya Katiba.

 • VYOMBO VYA KIKATIBA

Tume imependekeza baadhi ya vyombo vifuatavyo viwe vya Kikatiba; Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali, Baraza la Mawaziri, Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri; Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, Tume Huru ya Uchaguzi, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora

 • MAADILI YA VIONGOZI NA MIIKO YA UONGOZI

Tume inapendekeza maadili ya viongozi wa umma, pamoja na miiko ya uongozi yawekwe kwenye Katiba. Tume pia imependekeza kuwa Sekretariati ya Maadili ibadilishwe kuwa Tume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.

 • HAKI ZA BINADAMU

Tume inapendekeza kwamba vikwazo vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.

Tume pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya wafanyakazi, , haki ya mtoto, haki za Watu wenye Ulemavu, Haki za Wanawake, Haki za Wazee, Haki za Makundi Madogo katika Jamii, Haki ya Elimu na Kujifunza, Haki ya kupata habari, Haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na kadhalika.

 • URAIA

Tume imependekeza kwa kutaja Raia wa Jamhuri ya Muungano na haki zake.

 • MIKOPO NA DENI LA TAIFA

Tume imependekeza kuwa, Serikali itawajibika kutoa taarifa Bungeni kuhusu Mikopo kwa kuainisha kiasi cha deni lililopo, riba yake na matumizi ya fedha za Mikopo na utaratibu wa kulipa Madeni ya Taifa.

 • MFUMO WA UTAWALA

Tume inapendekeza Tanzania iendelee na mfumo wa Jamhuri kwa maana ya nchi inayoongozwa na Rais Mtendaji ambaye ni Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

 • UCHAGUZI WA RAIS

Tume inapendekeza Rais aendelea kuchaguliwa na wananchi na pamoja na sifa nyingine, mtu anayeomba urais asiwe chini ya miaka 40.

Tume imependekeza Mgombea Urais anaweza kupendekezwa na Chama cha Siasa au kuwa Mgombea Huru.

Mgombea wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa Mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi. Wanaoweza kufungua kesi ni wagombea Urais. Aidha, ni Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na Mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku therathini.

Rais aliyeshinda ataapishwa siku thelathini tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na Mahakama.

 • MADARAKA YA RAIS

Tume inapendekeza kwamba, Rais abaki na madaraka ya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Hata hivyo inapendekezwa Rais ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi. Kwa mfano:

Uteuzi wa Mawaziri na Manaibu Waziri, Rais atateua na Bunge litathibitisha.

Kuhusu Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu Rais atawateua kutokana na majina ya watu waliopendekezwa na Tume ya Uutumishi wa Mahakama na baada ya hapo Bunge litathibitisha.

Tume inapendekezwa kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa, ambalo kati ya majukumu yake itakuwa ni kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kuhusu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma.

 • KINGA YA RAIS

Tume inapendekeza Rais abaki na kinga kama ilivyo sasa na anaweza kushitakiwa na Bunge kama ilivyo Katiba ya sasa.

 • IDADI YA MAWAZIRI

Tume imependekeza Rais aunde Serikali ndogo iliyo na Mawaziri wasiozidi kumi na tano na mawaziri hao wasiwe wabunge. Mawaziri hawatahudhuria vikao vya Bunge isipokuwa kama watahitajika kutoa ufafanuzi kwenye kamati za Bunge.

 • BUNGE

Tume imependekeza wabunge wa aina mbili. Wabunge wa kuchaguliwa na wabunge watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha Watu wenye Ulemavu.

Kila Jimbo la Uchaguzi litakuwa na Wabunge Wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.

Tume inapendekeza kwamba, Mbunge akifukuzwa na Chama cha Siasa abaki kuwa Mbunge lakini akihama Chama atapoteza Ubunge wake.

Tume imependekeza ukomo wa Ubunge uwe vipindi vitatu vya miaka mitano mitano. Hata hivyo, wananchi wanaweza kumwondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi chake.

Tume imependekeza kusiwepo na uchaguzi mdogo isipokuwa kama nafasi inayokuwa wazi inatokana na Mbunge huru ndipo utafanyika uchaguzi mdogo kujaza nafasi hiyo, lakini kama nafasi ikiwa wazi kutokana na Mbunge wa Chama cha Siasa basi nafasi hiyo, ijazwe na mtu kutoka Chama hicho.

Inapendekezwa Spika na Naibu Spika wasitokane na Wabunge na wasiwe Viongozi wa vyama vya Siasa.

 • TUME YA UCHAGUZI

Tume inapendekeza jina la tume liwe Tume Huru ya Uchaguzi. Tume pia inapendekeza sifa za wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ziwekwe kwenye Katiba. Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi watapatikana kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa ndani ya Katiba kwa kuomba. Majina ya waombaji yatachambuliwa na Kamati ya Uteuzi ambayo Mwenyekiti wake atakuwa Jaji Mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni Majaji Wakuu wa nchi Washirika, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Maspika wa Mabunge wa nchi Washirika na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu.

Inapendekezwa Tume huru ya Uchaguzi isimamie masuala ya uchaguzi, kura ya maoni na Usajili wa Vyama vya Siasa.

 • MAHAKAMA

Tume imependekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) Majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

 • MUUNDO WA MUUNGANO

Tume imependekeza mfumo wa Serikali tatu. Yaani Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 • ORODHA YA MAMBO YA MUUNGANO

Tume imependekeza katika Rasimu ya Katiba kuwa orodha ya Mambo ya Muungano yawe 7 badala ya 22 yaliyopo sasa.
Mambo ya muungano yanayopendekwa ni:

 1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 2. Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 3. Uraia na Uhamiaji
 4. Sarafu na Benki Kuu
 5. Mambo ya Nje
 6. Usajili wa Vyama vya Siasa
 7. Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
 • BENKI KUU

Tume imependekeza Muungano wa Shirikisho kutokana na uzito wa maoni ya wananchi. Hivyokutakuwa na Benki Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya Sarafu na Fedha za Kigeni na Benki za Washirika wa Muungano.

 • BENKI ZA SERIKALI ZA WASHIRIKA

Tume imependekeza kuwepo kwa Serikali ya Shirikisho la Nchi tatu, inapendekezwa kuwepo kwa Benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti ya fedha za Serikali za kila Mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki za biashara katika mamlaka zao.

   3. BAADHI YA MAMBO AMBAYO HAYAMO KWENYE RASIMU YA KATIBA

 • Serikali ya Majimbo
 • Mahakama ya Kadhi
 • Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
 • Serikali za Mitaa
 • Uraia wa Nchi mbili

Advertisements