VIDEO:- HATUTAPIGWA, HATUTALIA WALA KULALAMIKA TENA; CHADEMA

  • Wasema Watashinda Kwa Kishindo na kutaja asilimia.

  • Wamshanga Mwigulu Nchemba kwa siasa ambazo zinamuhusisha Mwenyekiti wa chama chake.

  • Wataja vikosi vyao vya kujilinda na kusema ndiyo mwisho wa kuonewa.

JESHI LA POLISI NA SERIKALI WAJIULIZE WAMETUFIKISHA VIPI HAPA?
Badala ya kuipiga mikwara CHADEMA na kuwatishia viongozi wake uongozi wa jeshi la polisi na Ikulu inapaswa wawe na ujasiri wa kusimama mbele ya vioo na kujiuliza maswali ambayo majibu yake yagonge visogo vyao. Maswali hayo baadhi yake ni haya:

  1. Kwanini CHADEMA imefikia mahali pa kutaka kujilinda?

  2. Vyombo vya usalama vimepungukiwa nini kiasi kwamba chama kikuu cha upinzani nchini haiviamini?

  3. Je, uongozi wa vyombo vya usalama una mahusiano gani ya kikazi na viongozi wa CHADEMA?

  4. Je, ni kwanini matukio yaliyotokea na kugusa CHADEMA hayachunguzwi kwa kasi ile ile kama matukio mengine – mfano mauaji ya Padre Mushi kule Zanzibar yamepewa uzito wa uchunguzi (Hadi Rais kaingilia kati) kuliko mauaji ya wanawake na mtoto mdogo Arusha?

  5. Je vyombo vya usalama vinaweza kuchukua hatua gani kurudisha imani ya CHADEMA na wanachama wake kuwa vinafanya kazi kwa weledi na siyo kama sasa ambavyo vimebatizwa majina ya CCM kama PoliCCM (badala ya Polisi), na TICCM (Badala ya TISS) n.k?

  6. Rais Kikwete ajiulize kwanini wale aliowakabidhi dhamana ya kusimamia usalama nchini wameifikisha nchi hapa – kuwalaumu CHADEMA kwa kujilinda ni kukosa umakini na kuwa na usahaulifu unaobagua (selective amnesia).

BY:- Mwanakijiji….

Haki ya kujilinda ni miongoni mwa haki za msingi kabisa za binadamu ambazo zinatokana na mtu kuwa binadamu na haziwezi kuondolewa au kufutwa na chombo chochote. Ni haki ambayo mwanadamu anayo kwa kuzaliwa kwake. Haki hii kwa kadiri tunavyokua tunaiacha kwenye vyombo mbalimbali lakini mwisho wa siku bado ni haki yetu ya msingi kama binadamu. Mwanadamu anaposhambuliwa ana haki ya kujikinga kukinga maisha yake na mali yake; na kama ni familia yake inashambuliwa ana haki ya kulinda familia yake. Huwezi kumwambia mtu kuwa akipigwa ainame na kukubali kipigo bila kujilinda.

Haki hii ni tofauti na haki ya kujitetea au kulipiza kisasi – japo ni haki zinazoendana pamoja katika ile haki ya msingi ya kutokudhulumiwa. Haki ya kujilinda ni haki ambayo mtu si lazima alipe kisasi lakini ni haki ya kuzuia kutendewa vibaya. Hii ndiyo sababu watu wamejenga kuta kwenye nyumba zao, wameweka vyombo vya ulinzi na kuajiri walinzi. Wote hawa wanatumia haki yao ya kujilinda bila kulazimika kulipa kisasi. CHADEMA kama chama cha siasa ambacho tayari kimeshadhurika mara kadhaa sasa na kwa niaba ya wanachama wake kimeamua kutoa mafunzo ya ukakamavu na kujilinda; wanatumia haki hii ya msingi.

Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama na wale wote wanaobeza wanahitaji kutafakari upya kama wao wangekuwa upande wa pili kama wasingetafuta mbinu ya kujilinda. Kama wale watu waliowekwa kutoa ulinzi ndio hao hao wanaoharibu ulinzi utakuwa ni ujinga wa hali ya juu kuwategemea. Bila mabadiliko ya msingi ya mfumo na utendaji wa jeshi la polisi katika mazingira ya vyama vingi vya siasa ni vigumu kwa chama cha upinzani kama CHADEMA kuweka maisha yake na maisha ya viongozi wake mikononi mwa chombo hicho. Ni wajibu na ni haki kwa wao kufikiri namna ya kujilinda na kulinda maslahi yake. Hili halihitaji baraka kutoka CCM, Ikulu, au Polisi.

Advertisements