KWANINI SI MUUMINI WA SERIKALI TATU: MWANAKIJIJI

MWANAKIJIJI

Aprili 30, 1992 aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais John Samwel Malecela alitoa hotuba ndefu Bungeni ambapo alipinga hoja ya serikali tatu. Kwanza alipinga kwa sababu tume ya Nyalali ilipata asilimia 49 tu ya watu 36299 waliotoa maoni walitaka serikali tatu. Kwamba watu karibu 17,000 ndio walitaka serikali tatu na kwa hilo tu tume ikapendekeza serikali tatu. Hata sasa suala la serikali tatu hatujaambiwa ni watu wangapi wanataka hilo kwenye tume ya Warioba hadi Tume iliingize kwenye rasimu ya Katiba. Na idadi hiyo inaendana vipi na wale wengine waliotaka mifumo mingine ya serikali.

Malecela alisema kwa uthabiti hivi:

Sisi hatuoni kuwa kuna hoja ya kisheria na ya kisiasa ya kubadili mfumo wa sasa wa Serikali mbili na kuanzisha mfumo wa Serikali tatu. Tunaamini kuwa mfumo wa Serikali tatu, utadhoofisha Muungano wetu kisiasa na kiuchumi.
Nyerere akielezea hili kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (UWHT) anasema hivi:

Waziri Mkuu aliisahau hotuba hii; na wabunge waheshimiwa walisahau shangwe zao na
makofi yao. Wakapitisha Bungeni, “kwa kauli moja”, Azimio la kutaka Serikali ya Tanzania ilete
muswada wa kubadili Katiba ya Nchi yetu ili kuwa na Serikali ya Tanganyika “ndani ya Muungano”,
kwa madai ya kwamba hayo ndiyo ” matakwa ya wananchi wa Tanzania.
Lakini ukweli wa suala hili unabaki pale pale: Wananchi wa Tanzania hawadai Serikali ya Tanganyika;
na mimi nasema, ukifufua Tanganyika, utaua Tanzania. Fahari wawili hawakai zizi moja: “Yeltsin”
wa Tanganyika’ ataua Muungano. Lakini pia sababu zile zile za ukabiIa na udini na tamaa za
uongozi zitakazoua Tanzania hatimaye zitaiua Tanganyika nayo.

Nyerere aliona – na mimi nakubaliana naye – suala la kudai Tanganyika wakati ule kama ilivyo leo ni suala la tamaa ya uongozi na matokeo yatakuwa ni yale yale.

Nyerere aliona kuwa watu wa Tanzania wanachotaka ni kuwadhibiti viongozi wao. Yeye aliona kwa usahihi kabisa kuwa kuleta Tanganyika haitatatua tatizo la viongozi wahalifu kwani sasa utakuwa na viongozi wabovu kwenye Muungano na wengine kwenye Tanganyika na Zanzibar. Alisema suala basi ni kuweka utaratibu wa kuwawajibisha viongozi sawasawa.

Nyerere akaelezea vizuri kwanini wakati wa Muungano hatukwenda kwenye serikali moja au kwenda serikali tatu. Alisema hivi:

Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa
mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na
ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi
na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza
Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tutuhumiwe hata kwa makosa,
kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!

Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama
kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha
Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa
Tanganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tanganyika ingeendesha Serikali
yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la
watu 12,300,000.

Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo
ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na
wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya
Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika.

Ni vizuri kuangalia hizo namba leo hii; Zanzibar ina watu kama milioni 1.3 na Bara kuna zaidi ya watu milioni 45. Hivyo serikali tatu kwa mantiki ya Nyerere bado Tanganyika itabeba mzigo mkubwa zaidi – kuwa na serikail ya kuhudumia watu milioni 45 na pia kuchangia mchango mkubwa kwa serikali ya watu milioni 46.3.

Nyerere alikutana na viongozi wa chama na wabunge wa CCM na kuwashawishi kuipinga hoja ya serikali tatu na serikali nayo. Lakini alipoondoka kwenye Asia akiwa kwenye ziara ya Nchi za Kusini (alikuwa Mwenyekiti) huku nyuma serikali na viongozi wakashindwa kupinga kwa hoja maridhawa kabisa serikali tatu (kama tunavyoona sasa). Nyerere aliandika kwa ukali na uwazi hili tena kwa mshangao. Alisema:

Nilipouliza kwa nini hawakupinga hoja ya Serikali tatu kama tulivyokuwa tumekubaliana majibu ya viongozi wetu wakuu yalikuwa ni ya ajabu kabisa. Ati wabunge wenye hoja baada ya kuonana na mimi Msasani walikwenda Bungeni wakiwa wakali kama mbogo! Tena walikuwa wakiwatukana wenzao (yaani wabunge wa Zanzibar) kwa kuwataja majina.

Hizi ni sababu za ajabu sana za kuwafanya viongozi watu wazima watelekeze msimamo mzima wa Chama chao na makubaliano ya watu makini kuutetea msimamo huo na waamue kuikumbatia hoja ya mbogo wakali! Huu ni uongozi wa ajabu kabisa!

Nyerere alifikia hitimisho ambalo hata leo tunaliona. Watu wanataka serikali ya Tanganyika kwa sababu wamechoka na Wazanzibari. Nyerere anasema hivi:

Ndivyo viongozi wetu waheshimiwa wanavyojaribu kufanya hata katika suala hili la Muungano.
Wanataka kuvunja Tanzania maana “wamechoka na Wazanzibari”; lakini hawataki kusema hivyo wazi wazi. Wanachosema ni kwamba wanataka Serikali ya Tanganyika “ndani ya Muungano”, ingawa wanafahamu, maana si watu wapumbavu, kwamba ukifufua Tanganyika utaua Tanzania.

Muundo wa Muungano unabadilika na si lazima uwe serikali tatu
Mimi siamini katika serikali tatu kwa kiasi kikubwa kwa sababu zile zile za Nyerere. Lakini pia ninaamini kuwa wananchi ndio wana haki ya kuamua mfumo wa Muungano na hata uwepo wa Muungano wenyewe. Sasa hivi watu wanajadili serikali tatu kwa sababu wamekatazwa kujadili kuuvunja Muungano! Watu wamekubali kuwa ni lazima tuungane hivyo tutafute namna ya MUungano. Mimi naamini wananchi ndio wanapaswa kuamua kwanza kama Muungano uwepo na wakishaamua hivyo uwe wa namna gani.

Nyerere anasema hivi:

Muundo wa Muungano, pamoja na kwamba hatutaki uwe ukitibuliwatibuliwa mara kwa mara, ni suala
la sera, si amri ya Mungu. Vyama vya siasa mbalimbali vinaweza vikawa na maoni mbalinbali kuhusu
muundo unaofaa kwa Katiba ya nchi yetu. Muundo utakaokubaliwa na wananchi walio wengi ndio
utakaokuwa sehemu ya Katiba ya nchi yetu. Muundo wa Serikali mbili unakubaliwa na wananchi,
lakini unatokana na sera ya TANU na ASP, na kwa sasa CCM. Chama Cha Mapinduzi kikipenda
kinaweza kubadili sera hiyo ya muundo wa Serikali mbili bila kuuliza wananchi kwanza. Kinaweza
kufunya hivyo kwa kuhisi kuwa hivyo ndivyo wananchi wengi watakavyo; lakini pia kinaweza kufanya
hivyo kwa sababu kinaamini kuwa inafaa kufanya hivyo, hata kama wananchi wengi hawakudai au
hawapendi mabadiliko.

Na Hapa chini ndio msimamo wangu vile vile: Kwanini tunalazimishwa kujadili serikali tatu. Kwanini tumesalimu amri na kufikiria serikali tatu? Kwanini CCM wameamua tujadili serikali tatu na sisi tunajadili serikali tatu. Hivi kweli watu wanafikiria hili wazo la serikali tatu limetokana na wananchi kwenye maoni ya tume ya Warioba au ni carryover ya mjadala wa 1992?

Nyerere anasema:

Nasema, niliamini kuwa ni kosa kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kukubali chama kiulize wananchi
kama inafaa tuwe na Serikali Tatu. Kwanza, kwa sababu hiyo niliyoeleza; na pili, hata kama CCM
ingependa kubadili sera yake, kwa nini turukie Serikali Tatu? Kwa nini tusitake maoni ya wananchi
kuhusu Serikali Moja! Au hata kuhusu SerikaIi za Majimbo? Tumejadili katika vikao gani
tukakubaliana kuwa miundo mingine yote haifai ila muundo unaofaa ni ule wa Serikali Tatu? Au hata
Bunge lenyewe, limejadili miundo mbali mbali ya Muungano katika kikao gani hata wabunge
waheshimiwa pamoja na waheshimiwa mawaziri wetu wakafikia uamuzi baada ya mjadala kwamba
muundo peke yake unaofaa ni huu wanaopendekeza, wa kuwa na Serikali Tatu?

Na maneno haya ya Nyerere yasikike kwenye masikio yaliyoziba ya watawala wetu walioshindwa!

Hizi zote ni mbinu za viongozi wetu waheshimiwa kutaka kukiingiza Chama katika njia moja tu
nyembamba, na kutuburura kama vipofu tuitumbukize nchi yetu shimoni. Ni jitihada za kukifanya
chama na sisi wengine wote tukubali msimamo wao wa kutaka kuigawa nchi yetu.

Serikali tatu haitotatua matatizo ya Muungano itayaongeza tu. Tunaopinga serikali tatu hatupingi kwa sababu ya gharama tu – hili ni jambo dogo zaidi lakini tunapinga kwa sababu ya mantiki nzima ya kuwa na serikali tatu na nchi mbili! lakini wenzetu wanataka tuwe na nchi mbili na serikali tatu!

Mimi napinga serikali tatu – naamini kama kweli watu wanataka tuimarishe Muungano basi ni kuunda nchi moja, serikali moja mifumo mbalimbali au utengano! Kwani nani kasema ni lazima tuungane? Hatutakuwa nchi ya kwanza duniani kuvunjika na watu kuendelea kuishi pamoja na ujirani mwema.

mwanakijiji@jamiiforums.com
The Best of Tanzanian Socio-Political Blogging – http://www.mwanakijiji.com
Advertisements