RIDHIWANI AWABEZA WAANDISHI WA HABARI

 

35 36e8f

Katika toleo  la Gazeti la NIPASHE   Juni 18, 2014, kulikuwa na habari iliyoanzia ukurasa wa kwanza na kuendelea wa tano iliyobeba kichwa cha habari: Ridhiwani kijana asiyekuwa na shukurani.

Habari hiyo ilikuwa ikizungumzia matamshi ya Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete, akiwaponda wanahabari nchini kuwa asilimia kubwa ni makanjanja na kwamba wanapoandika habari wanasukumwa na weledi wa jinsi wanavyofikiria vichwani na itikadi zao za kisiasa.

Ridhiwani alitoa kauli hiyo Juni 8, mwaka huu wakati wa mahafali ya wanafunzi ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika vyuo vikuu vya mjini Morogoro, yaliyofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Umwema, mjini humo.

Alisema waandishi wengi hapa nchini wanasukumwa sana na utashi wa siasa zao, jinsi wanavyofikiria vichwani mwao na itikadi ya siasa. Aliongeza kuwa wakati mwingine hata jambo zuri likifanyika haliwezi kusifiwa badala yake kazi yao kubwa ni kuandika mambo ya ovyo ovyo tu.

Mbunge huyo alidai kuwa, asilimia kubwa ya waandishi nchini ni makanjanja na wanapokaa kwenye meza zao wanaandika vitu tu, wanapikapika vitu, akimaanisha wanaandika vitu vya kutunga.

Sisi tumeshangazwa sana na kauli ya mbunge huyu kijana ambaye ni miezi michache tu iliyopita amechaguliwa kushika nafasi hiyo kuwakilisha wananchi wa Chalinze.

Tunasema tumeshangazwa na kauli hiyo, kwa sababu Ridhiwani akiwa mwanasiasa kijana, anapaswa kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika taifa hili ambalo linakabiliwa na changamaoto nyingi za umasikini, badala ya kuwabeza.

Tunafahamu kuwa ni ukweli usiopingika kuwa tasnia ya habari nchini inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini hiyo siyo sababu ya mtu kama Ridhiwani ambaye ni mwanasiasa na tena Mbunge kutumia lugha ya kejeli na kudhalilisha tasnia hiyo, badala ya kuwa sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo.

Kama amesahau, labda tumkumbushe Ridhiwani kwamba, ni vyombo vya habari na waandishi wa habari ambao leo anawabeza, wametoa mchango mkubwa katika kuchaguliwa kwake kuwa Mbunge wa Chalinze hivi karibuni tu.

Ridhiwani alikuwa akizunguka na waandishi wa habari huku na huko katika jimbo zima la Chalinze waweze kuandika habari zake.

Ni waandishi wa habari hawahawa anaowabeza wamemsaidia kwa kiasi kikubwa Mbunge huyu katika kampeni hizo, wakitangaza na kueneza sera za chama chake na ahadi zake ili kuwashawishi wananchi wamchague, na kweli alifanikiwa na sasa ni Mbunge.

Ni Ridhiwani huyu huyu ambaye siku anaenda kuapishwa bungeni mjini Dodoma baada ya kuchaguliwa, anadaiwa kubeba rundo la waandishi wa habari kwenda kushuhudia kuapishwa kwake.

Leo tunashangaa kuona akitoa lugha zinazotaka kuaminisha watu kuwa waandishi wa habari ni watu wa ovyoovyo, wasiopaswa kuaminiwa katika jamii.

Ridhiwani amebeba hulka ile ile ya baadhi ya wanasiasa ambao huwatumia waandishi wa habari kufanikisha mambo yao, lakini wanapofanikiwa huanza kuonyesha kiburi, dharau na kutoa kauli za kudhalilisha dhidi yao.

Kama kweli Ridhiwani ana nia njema na waandishi wa habari, angekuwa mstari wa mbele kutumia nafasi yake ya ubunge aliyoipata, kuibana na kuishinikiza serikali kupeleka haraka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari na sheria ya uhuru wa kupata habari viweze kusimamia sekta hii muhimu, badala ya kutumia lugha za kejeli na kudhalilisha.

Tunamshauri mwanasiasa huyu kinda atambue kwamba ndiyo kwanza ameanza kutembea katika ulimwengu wa siasa, ajifunze kutafakari kabla ya kusema. Daima kuweka akiba kwa kila jambo ni busara zaidi. Ridhiwani aache kuvimba kichwa kwani kitapasuka mapema.

CHANZO: NIPASHE

Advertisements