UCHAGUZI MKUU CUF NI JUNI 23 – 27 BLUE PEARL UBUNGO, DAR ES SALAAM

CUF

ZIKIWA zimebakia siku mbili ili Chama cha Wananchi (CUF) kifanye mkutano mkuu wa kuwachagua viongozi wa juu wa kitaifa, imebainika kuwa hali si shwari ndani ya chama hicho.

Tanzania Daima limedokezwa jana kuwa hali hiyo imesababishwa na kujiengua kwa Machano Khamis Machano aliyetaka kutetea nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti.

Habari za kuaminika kutoka CUF zinasema kwamba awali waliogombea nafasi hiyo ni Juma Duni Haji na Machano ambaye alijitoa kwa sababu ya afya yake kudorora.

Taarifa hizo zilisema baada ya kutangaza kujiengua katika kinyang’anyiro hicho mjini Zanzibar, ‘wapambe’ wake walionyesha kutoridhika.

“Ukweli kuhusu Machano kujitoa katika kinyang’anyiro ni huu… mwenyewe kwa kauli yake wakati anarejesha fomu alisema anajiengua kutokana na hali yake ya kiafya, hivyo hataweza kuhimili tena mikikimikiki ya uchaguzi na uongozi,” alisema mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu la CUF.

Bila kumung’unya maneno, mjumbe huyo alisema kwa miaka kadhaa sasa Machano anasumbuliwa na maradhi ya sukari yanayomfanya ashindwe kufanya shughuli za Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

“Hivyo nataka niwataarifu wanaCUF wenzangu wanaosema mzee Machano ameshinikizwa kuachia nafasi hiyo na wapambe wa babu Duni si kweli… kila mtu alikuwa na nguvu yake katika kinyang’anyiro hicho,” alisema mjumbe huyo.

Habari za ndani zilieleza kwamba jana kilifanyika kikao cha kupitisha majina ya wagombea mbalimbali huku Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba akipata upinzani kutoka kwa wagombea wawili waliojitokeza.

Katika nafasi ya uenyekiti wa CUF taifa waliojitokeza ni Chief Lutayosa Yemba kutoka Shinyanga na Mbezi Adam Bakari wa Temeke, Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Maalim Seif Shariff Hamad hakupata mpinzani na hivyo kuiacha nafasi hiyo wazi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo, alithibitisha kuwa maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika na kwamba utafanyika kuanzia Juni 23 hadi 27 katika Hoteli ya Blue Pearl Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Advertisements