“LEO SAA MBOVU IMEPATA MAJIRA?” FID Q

Farid Kubanda ‘Fid Q’

MKALI wa muziki wa hip hop nchini, Farid Kubanda ‘Fid Q’, amesema tuzo za mwaka huu za Kili zilikuwa za mwisho kushiriki endapo waandaaji wasingetambua mchango wake tangu mwaka 2004.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Fid Q alisema miaka mingi amekuwa akishiriki tuzo hizo bila mafanikio yoyote. Kwamba tangu alivyopata mwaka 2004 hajawahi kupewa tena wakati kazi alikuwa anafanya na kuambulia kushiriki tu.

“Sijawahi kumwambia mtu, nilikuwa nasema mwenyewe moyoni na ndiyo maana hata siku ile nilishindwa kuongea nilipotakiwa kuongea, nilitaka kuwauliza leo saa mbovu imepata majira? Lakini nikaona kwa sababu wenyewe wamejiongoza na kuona mchango wangu, basi niwaache tu,” alisema.

Fid Q alisema kutokana na upinzani uliopo katika soko la muziki kwa sasa, wasanii wengi wamekuwa hawapendani, na yeye hana mpango wa kugombana na mtu na anayemchukia hana mpango naye.

“Sijawahi kugombana na msanii yoyote, mimi kila msanii ni mshikaji wangu, ambaye ataona ana chuki na mimi kwa mambo yake binafsi mimi sijali, mimi kila msanii ni ndugu yangu,” alisema.

Fid Q mwaka huu alitwaa tuzo mbili za msanii bora wa kiume hip hop na mtunzi bora wa mashairi ya hip hop.

Advertisements