CHADEMA WAJIBU MAPIGO, SASA WAMTAKA CAG KUWEKA WAZI RIPOTI ZA HESABU ZA MAPATO NA MATUMIZI YA VYAMA VYA SIASA

CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuweka wazi ripoti za hesabu za mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini, kwa ajili ya kusimamia misingi ya uwajibikaji.

Kimesema siku zote kimekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi ndani na nje ya chama, hivyo kwa upande wake hakina hofu yoyote ya ripoti za ukaguzi wa hesabu hizo kuwekwa wazi.

Pia kimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kujiandaa kupokea maandamano ya wanachama na viongozi halali wa CHADEMA watakaofika ofisini kwake kumpatia ukweli na kukitetea chama chao dhidi ya propaganda ambazo zimefikishwa kwake na watu kiliodai ni mamluki na masalia ya wasaliti, baada ya viongozi wao kufukuzwa uanachama mapema mwaka huu.

Akizungumza na Tanzania Daima mjini Dodoma jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano wa chama hicho, John Mnyika, alisema kama Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ameamua kuwa ‘mpokeaji’ wa maandamano, basi ajiandae kwa maandamano makubwa ambayo yatabeba ujumbe wenye hadhi ya CHADEMA badala ya hoja za kipuuzi alizopelekewa hivi karibuni.

Mnyika alikuwa akijibu maswali ya gazeti hili, lililotaka ufafanuzi zaidi kutokana na kauli zake alizotoa mbele ya waandishi wa habari juzi mjini Dodoma alipokuwa akitoa msimamo wa CHADEMA kuhusu madai ya kundi la watu waliofika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na CAG, wakidai wao ni wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho.

Kabla ya kwenda ofisi hizo mbili, watu hao walifanya mkutano na waandishi wa habari Juni 23, mwaka huu ambapo pia, bila kuonyesha vielelezo, walidai kuwa wao ni wajumbe wa vikao vya CHADEMA.

Katika hali ambayo inatia shaka uhalali wa ujumbe wao, siku moja baada ya mkutano huo, baadhi ya watu ambao majina yao yalionekana kuandikwa kwenye orodha, walianza kukanusha kuwa hawahusiki na kundi hilo, na kwamba wao ni wanachama watiifu kwa CHADEMA, na kwamba hawajui majina yao na saini zao viliwekwa kwenye orodha hiyo kwa nia gani.

“CHADEMA kama taasisi, si chama cha ufisadi wala ubadhirifu. Ni chama kinachoshirikiana na vyama vingine kuongoza Watanzania kwenye mapambano dhidi ya ufisadi na ubadhirifu. Chama hiki hakiwezi kuvumilia ufisadi na ubadhirifu wa aina yoyote, iwe nje au ndani ya chama, ndiyo maana sisi ndio tuliotaka sheria ibadilishwe, utaratibu ubadilishwe, ili CAG akague mahesabu ya vyama vya siasa.

“Baada ya sheria kutungwa, udhaifu wa Ofisi ya Msajili, Ofisi ya CAG na Serikali ya CCM, umefanya kwa miaka mingi mahesabu yasikaguliwe. Zilipozuka hoja za ukaguzi wa hesabu, mzigo ukitaka kuhamishiwa kwa vyama, kama vile vyama havitaki, tukalielezea suala hili. Hatimaye CAG akafanya ukaguzi.

“Sasa hawa wamemuandikia mkaguzi wakitaka ripoti ya CHADEMA, mimi kama msemaji wa chama, nitoe mwito kwa CAG kuweka wazi ripoti za vyama vyote alivyovikagua.

“Aweke wazi kwa haraka kadiri inavyowezekana. Kwa sababu Bunge limeshaarifiwa kuwa mkaguzi amemaliza kufanya ukaguzi kwa baadhi ya vyama na vingine havijakaguliwa. Vile ambavyo havijakaguliwa vitajwe kwa majina na vikaguliwe. Halafu sasa tuone  hayo madai ya mara Mbowe hivi, mara Slaa hivi,” alisema Mnyika.

Advertisements