KAZI YA UKAGUZI NA URASIMISHAJI WA KAZI ZA MUZIKI NA FILAMU LAANZA; TRA

Mamlaka ya mapato Tanzania ‘TRA’ imetoa tangazo kwa tasnia za sanaa ya filamu,muziki, kwa kuanza zoezi la urasimishaji wa kazi za wasanii kwa kuanza kukagua bidhaa za wasanii na kuziwekea stika.

10431899_340541062760789_1672094960_n

Taasisi za Serikali zilizokabidhiwa jukumu la kushughulikia urasimishaji wa tasnia za sanaa ya muziki na filamu, zimeanza rasmi zoezi la kukagua na kukamata bidhaa zote za muziki na filamu ambazo hazina sifa ya kuuzwa na kusambazwa katika soko la ndani na kupelekwa nje ya nchi.

Sheria ya Ushuru wa Bidhaa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, na kupitishwa kwa kanuni zake mwaka 2013 inamtaka kila mfanyabiashara wa bidhaa za muziki na filamu kuhakikisha kuwa bidhaa zote za muziki na filamu zinawekewa stempu za Ushuru wa Bidhaa zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya kusambazwa.

Taasisi za Serikali zinazohusika katika zoezi hili ni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania (TFCB), Chama cha Hakimiliki na Hakishirikishi Tanzania (COSOTA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikitoa elimu kwa wadau wote wanaojihusisha na utengenezaji, uaigizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa zinazohusika na muziki na filamu pia kuhakikisha kuwa wanakamilisha mchakato wote wa uwekaji stempu za Ushuru wa bidhaa kwa kazi zinazoingizwa katika soko la ndani na zinazosafirishwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa sheria wahusika wote wa uzalishaji, uagizaji toka nje ya nchi na usambazaji wa bidhaa hizo wanatakiwa kufika kwa taasisi hizo ili kusajiliwa na kukamilisha utaratibu wa kusajili na kukaguliwa kwa kazi husika kabla hazijapatiwa stempu za Ushuru wa bidhaa kwa ajili ya kubandikwa kwenye kazi husika.

Utaratibu unawataka wale wote wanaokusudia kushughulika na kazi za muziki kuanzia BASATA na baada ya hapo kufika COSOTA ambapo huko hupewa vibali kabla ya kwenda TRA ili kununua stempu. Kwa kazi za filamu wahusika wanatakiwa kwenda Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kabla hawajapeleka kazi husika COSOTA na baadaye TRA kwa ajili ya ununuzi wa stempu.

Stempu hizi zinapatikana ofisi za Idara ya fedha, Makao Makuu ya TRA. Kila kazi, yaani CD, DVD au kanda zinatolewa stempu mbili zenye namba moja katika mtiririko maalum wa namba (serial number). Stempu moja hubandikwa katika kasha na nyingine kwenye CD, DVD au kanda. Utaratibu unamtaka mhusika anayehitaji stempu kuwasilisha maombi tofauti kwa kila kazi husika. Hairuhusiwi kuweka stempu zilizoombwa kwa ajili ya kazi moja kwenye kazi nyingine hata kama kazi hizo zimetolewa na mzalishaji au msambazaji mmoja.

Aina za stempu na matumizi yake ni kama ifuatavyo:

  • Filamu toka nje ya nchi – rangi ya kijani (green).

  • Muziki toka nje ya nchi – rangi bluu (blue).

  • Filamu zilizotengenezwa ndani ya nchi – zambarau (violet)

  • Muziki wa ndani ya nchi – rangi ya pinki (pink)

Advertisements