NINA WASIWASI KAMA MWAFAKA AU MARIDHIANO YATAPATIKANA AGOSTI WAKATI BUNGE MAALUMU LITAKAPOKUTANA; BOMANI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Jaji Mark Bomani akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Jaji Mark Bomani akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Jaji mstaafu Mark Bomani amelishauri Bunge Maalumu la Katiba kuweka kando suala la muundo wa serikali kwa kuwa ndiyo chanzo cha mgawanyiko mkubwa baina ya wajumbe.

Pia amewashauri wajumbe wa Bunge hilo wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni ili mchakato huo uweze kuendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Jaji Bomani alisema suala la muundo wa Serikali licha ya kusababisha mgawanyiko limesababisha hoja nyingine muhimu kusahaulika. 

“Kwa bahati mbaya sana kwa maoni yangu, mjadala wa mapendekezo hayo umezua malumbano na ubishi mkali, kiasi cha kufanya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kujitoa,” alisema Jaji Bomani. 

Alisema amewahi kutoa maoni kwamba suala lote la muungano na idadi ya Serikali linatakiwa lijadiliwe kwanza ama na Serikali mbili zilizopo, yaani Zanzibar na ya Muungano au Wazanzibari waulizwe iwapo wanautaka muungano. 

“Hata hivyo nina wasiwasi kama mwafaka au maridhiano yatapatikana mwezi Agosti Bunge Maalumu litakapokutana, kwa kuwa zimejitokeza tofauti kubwa za kimtazamo au kiitikadi bila kusahau masilahi binafsi,” alisema Jaji Bomani. 

Alisema kwa uzoefu wake katiba nzuri kwa nchi yoyote ni ile ambayo imepatikana kwa wananchi wengi kuikubali na siyo vinginevyo.

“Katiba nzuri ni ya maridhiano. Katiba nzuri haiwezi kupatikana kwa wingi wa kura au hoja ya nguvu tu bali inatakiwa iwe inakubalika na walio wengi (consensus),” alisema.

Aliyataja mambo mengine muhimu ambayo yanapaswa kujadiliwa na wajumbe kuafikiana ni pamoja na suala la uwakilishi sawa wa jinsia yaani asilimia 50 kwa 50, kwenye ubunge na halmashauri za wilaya.

“Suala la mawaziri kutokuwa wabunge nalo pia nafikiri linaweza kujadiliwa na mwafaka ukapatikana, muundo wa tume huru ya uchaguzi na suala la mgombea binafsi nalo naamini linajadilika wanaoliogopa hawana msingi wa kufanya hivyo,” alisisitiza Jaji Bomani.

SOURCE:- Mwananchi

Advertisements