BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI NI USHAHIDI KUWA JK AMA HAJUI AU HAONI TATIZO LA WATENDAJI WAKE.

 • Raisi Jakaya Kikwete akimuapisha Waziri wa afya

  Kusuka upya ni kufumua kilichosukwa ovyo na kurudia au kusuka tena kwa lengo la kuboresha. Hata hivyo ni lazima anayefanya hivyo yeye mwenyewe ajue kwamba msuko wa kwanza ni ovyo au hauna mvuto.

 • Kuongezwa wapya wanne au watano katika kundi la wakuukuu 50 hakuwezi kuwafanya wale wakuukuu kuwa wapya.

 • Kuomba ridhaa ya kamati kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilikuwa njia ya kujitoa katika lawama kwa watakaoathirika na mabadiliko hayo.

Baada ya kamati za bunge kusema, bunge likasema, kamati ya wabunge ikasema na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ikasema, hapakuwa na sababu ya kubakiza baadhi ya mawaziri katika baraza lake teule(Baraza Jipya).

Hii ilikuwa fursa ya kufanya mabadiliko makubwa yakiongozwa na mchakato mkali wa uchunguzi wa wale ambao wangerejeshwa au kuteuliwa kwa mara ya kwanza katika baraza la mawaziri.

Hili halikufanyika na litamgharimu sana RaisiJakaya Kikwete pamoja na chama chake. Kosa la kwanza la kukosekana kwa mchakato makini limekwishaonekana.

Walioteuliwa kuwa mawaziri wameapishwa. Ni vigumu kukiri kuwa hili ni baraza jipya. Kuongezwa wapya wanne au watano katika kundi la wakuukuu hakuwezi kuwafanya wale wakuukuu kuwa wapya.

Wanabaki na ukuukuu wao. Upya katika hilo uko wapi?

Jipya ni ukubwa wake. Raisi Kikwete alipounda kwa mara ya kwanza Baraza la mawaziri mwaka 2006 lililokuwa na mawaziri 61.

Alipopigiwa kelele mwaka 2008 baada ya serikali yake kuvunjika bungeni, alipunguza hadi kufikia mawaziri 51.

Mwaka 2010 Raisi Kikwete aliunda Baraza la Mawaziri 51, lakini aliposhinikizwa, mwezi Aprili 2012 ameongeza hadi 55. Huu ndio upya uliopo.

Lililo wazi ni Raisi Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa shinikizo. Haikuwa hiari yake.

Walishinikiza aunde upya Baraza Lake. Kwa kuwakomoa akatengeneza baraza kubwa kuliko la mwanzo.Upo hapo mwananchi?

Uzito wa mzigo huu utaongezeka juu ya vichwa vya wananchi walipakodi.

Wananchi wanashuhudia watawala wao wakijirundikia ulaji mkubwa mpaka wanashindwa kujieleza.

Wengine wanatembea na silaha za kivita kulinda raslimali za nchi walizopora!

Ndiyo maana haikushangaza kuona watu waliokutwa na masanduku yaliyojazwa mali isiyojulikana wakiyalinda kwa silaha nzito nzito za kivita hawajashughulikiwa hadi leo!

Hivi kwa nini tunawalazimisha wananchi watufikirie kuwa tu sehemu ya uchafu huo? Huko alipopelekwa kwenye mazao, mbolea itapona kweli? Mchezo wa uporaji ukiendelezwa kilimo si kitakufa! Ukishawaua wakulima nchi inabaki vipi?

Kutokuwajibika kwa serikali ndiko kulikompelekea Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi kusimama kwenye bunge lililopita na kuziweka hadharani dhambi za mawaziri. Akasema, “Serikali ipo kama haipo.” Wizi unafanywa na serikali yenyewe.

Katika hali kama hiyo nani amkemee nani? Aliyetakiwa kuwa mkemeaji, ndiye mtetezi wa wezi. Kama siyo mshirika basi ni nani?

Jenerali Ulimwengu katika safu yake alinukuliwa akisema, “Sura iliyojitokeza ni kwamba hatuna serikali inayofanya kazi kama serikali, bali tuna mkusanyiko wa maofisa waliokabidhiwa ofisi mbalimbali ambazo wanazitumia kadri wanavyojua wao na wala hawana udhibiti wa kati.”

Akaongeza, “Tunachokishuhudia ni msambaratiko ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi hii, serikali iliyoparaganyika, mawaziri wenye kauli za kitoto, wakuu wa serikali wasiokuwa na maamuzi, waziri mkuu kivuli asiyekuwa waziri mkuu na mkuu wa nchi mtoro”

Kufichuliwa kwa wizi wa raslimali, ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyoainishwa na kamati za kudumu za Bunge na pia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kumeonyesha namna viongozi wote wenye jukumu la kusimamia mawaziri walivyoshindwa kazi.

Hali hii inaonyesha kwamba viongozi wanaowasimamia mawaziri ama ni legelege sana na dhaifu kiuongozi, au wao wenyewe ni sehemu ya uozo huo.

Kinachoongeza uchungu zaidi ni habari zilizofichuliwa kutoka ndani ya kikao kilichoitishwa ghafla kuwa mwenyekiti wa CCM eti alilazimishwa kujadili suala la mawaziri, uchafu wao na kutakiwa kwao kujiuzulu.

Habari zinasema mwenyekiti ambaye pia ni raisi  hakuwa  na nia ya kulijadili na wala halikuwa sehemu ya ajenda.

Kama Wabunge walitia saini zao kutaka kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ili ikiwezekana apoteze kazi yake, kitendo ambacho kingesababisha kuvunjika kwa baraza zima la mawaziri, kuipuuza hoja hiyo inashangaza.

Mwenyekiti anashangaza maana kama vyama vya siasa viliazimia kwenda kwa wananchi kukusanya saini zitakazotosha raisi mwenyewe kupigiwa kura kutokuwa na imani naye, kutochukulia hoja hii katika umuhimu unaostahili ni udhaifu wa kiwango cha kutisha.

Kasoro hii kubwa inanipeleka kujadili jingine kubwa katika uteuzi wake.

Kada maarufu wa CCM, George Mkuchika ameteuliwa kuwa waziri mpya ofisi ya raisi anayeshughulikia utawala bora.

Hili lina mapungufu makubwa. Ni kwa sababu kuu mbili. Kwanza, serikali hii inakabiliwa na tatizo kubwa la utawala bora. Mambo ya kiserikali, siri na taratibu zake, yanaenda ovyo.

Ni mwenendo huu ambao umefanya Mkuchika kuteuliwa kuwa waziri wa wizara inayohusika na idara nyeti kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Usalama wa taifa.

Bila uovyo katika wizara hii na vyombo vyake, Mkuchika asingeteuliwa kuwa waziri wa wizara hii labda kama lengo ni kumwezesha yeye kulipa visasi vya waliombanika akiwa TAMISEMI.

Tatizo la utawala bora katika miundombinu ya utawala wa serikali yetu, linahitaji mtu makini zaidi, mwadilifu zaidi, asiye na makundi na asiye na huruma za kifisadi.

Pili, Mkuchika ametokea TAMISEMI ambako hata raisi amesikika mara kadhaa akilalamika kuwa mambo yako hovyo mno na kuagiza halmashauri zichukue hatua kali.

Alisikika Dodoma akilalamika kwenye semina elekezi. Mara ya mwisho alilalamikia kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, mjini Tanga.

Baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kuonyesha uozo uliokithiri katika halmashauri zetu, hata kama Mkuchika aliukuta au hahusiki nao, ingetosha kutomteua katika nafasi nyeti kama hii.

Uteuzi wa Mkuchika ni dhihaka kwa CAG, Wabunge, kamati za bunge na hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Hata kama wananchi hawafahamu yote yaliyo nyuma ya pazia kuhusu uteuzi huu, raisi  ajue yeye ni mwanasiasa.

Hatimaye, kazi yake itafanywa kuwa ngumu kutokana na teuzi anazofanya bila kujali jamii inajua nini juu ya wateule wake.

Si ajabu kigezo muhimu kilichotumika kumteua ni hatua ya Mkuchika kuandika barua ya kujiuzulu bila kujitetea kama wengine.

Uteuzi mwingine tata ni ule wa Proffesa Jumanne Maghembe aliyehamishiwa wizara ya maji akitokea kilimo na chakula.

Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya kilimo na maji na uhusiano huo ungemwongoza raisi katika kufanya uteuzi wake kwa umakini wa ziada; hata wa kuazima.

Baada ya yeye mwenyewe na “swahiba” wake Lowassa kutofautiana juu ya nini kiwe cha kwanza, serikali ya Kikwete ilitangaza kilimo kiwe cha “kwanza” huku Lowassa akitangaza katika ziara zake kuwa elimu ndiyo “kwanza.”

Bila kujali tofauti zao binafsi tusizojua chanzo chake, tukubaliane kimsingi kuwa kilimo na maji ni vitu viwili muhimu. Aliyeshindwa Kilimo hawezi kuongoza Maji.

Ukiacha Mkuchika na Maghembe, hawa wawili ambao wamepigiwa kelele karibu na kila mtu, kikosi kizima hakina muunganiko.

Kwa Hawa Ghasia kupelekwa Tamisemi ni sawa na kupakia tembo kwenye pick up.

Hussein Mwinyi kupelekwa Afya licha ya kukiuka utamaduni mzuri wa Muungano, ni kuifungia wizara iache kufikiri tena.

Ni Mwinyi aliyegoma kujiuzulu wakati wa mabomu ya Gongo la Mboto na Mbagala; lakini akawa kinara wa kuwataka wenzie wajiuzulu.

Kuwabakiza mawaziri wanaotuhumiwa ufisadi, wizi na kushindwa kufanya kazi; na ambao vitendo vyao viovu vinaonekana kwa wengi, ni kuonyesha wazi kuwa mteuzi hana mawasiliano na wananchi.

Kwa naibu mawaziri, huko ni vurugu tupu. Baada ya kufichuka siri za jinsi wanavyovurugana na mawaziri wao, kuongeza idadi yao siyo tija, bali ni kuongeza gharama.

Mpaka sasa, hakuna kazi maalum ya naibu waziri inayojulikana, zaidi ya kujibu maswali yaliyoandikwa bungeni.

Gharama kubwa ya utitiri wa manaibu siyo suala la magari, ofisi, mishahara na ukwapuzi mwingine; bali muda wa raisi na waziri mkuu, ambao wanatumia kutatua migogoro ya watu hawa “wasio na kazi.”

Kwa hiyo utitiri wa manaibu ni kuongeza gharama za kikosi hiki dhaifu badala ya kuokoa jahazi lililokwishaanza kuzama.

Kwa haya, ongeza uteuzi wa manaibu kama Adam Malima, katikati ya kashfa nzito, tena za hivi karibuni; kukiwemo kukutwa na silaha ya kivita na ukimya uliofuatia.

Tukiuchekea utoto huu tunaikejeli amani yetu. Nasema hivi kwa sababu kufanyiwa mzaha jambo kubwa kama hili ni sawa na mwendawazimu kuchekea kitanzi ambacho kiko tayari shingoni mwake.

Kukubali kuongozwa kisaniisanii ni ukondoo, nalo ni tusi kwa yeyote aliye na akili timamu.

Kuibuliwa kwa kashfa ya Richmond kulisababisha baraza la mawaziri kuvunjika kwa mara ya kwanza katika awamu ya nne.

Baraza la mawaziri lilivunjika baada ya aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.

Akateuliwa Pinda kuchukua nafasi ya Lowassa na kisha baraza likasukwa upya.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 likaundwa baraza jingine, lakini hata kabla ya kufika nusu ya muhula wake limejiingiza katika ufisadi wa kutisha.

Hivi baraza hili litavunjwa mara ngapi? Kwanini hivi lakini? Tatizo ni mawaziri au mteua mawaziri?

Tatizo hapa siyo mawaziri wezi. Wezi wapo kila mahali hata katika hao wapya walioteuliwa wezi watakuwapo. Tatizo ni nchi kukosa kiongozi wa kusimamia mawaziri wezi ili wasiibe.

Kama tatizo ni kukosekana kiongozi wa kuwadhibiti mawaziri wasio waadilifu dawa yake si kuvunja baraza la mawaziri na kuunda jingine! Dawa ni kumpata kiongozi atakayeweza kuwadhibiti mawaziri wasio waadilifu.

Dawa ni kumpata kiongozi mwenye ujasiri na uwezo wa kuwafikisha katika vyombo vya sheria viongozi wote wanaotuhumiwa.

Kiongozi mwenye dhamana akishindwa kufanya hivyo anaonyesha udhaifu au ushirika wake katika kadhia hiyo.

Kwa baraza hili la mawaziri  Watanzania wanapaswa watambue ukubwa wa dhambi waliyoitenda wale waliowaficha ukweli mwingine.

Tuna miaka mitatu ya kwenda na hawa watu, kama kasi ya ubadhilifu ni kubwa kiasi hiki, hii nchi itabakiwa na kitu gani kufikia mwaka 2015?

Watanzania, huu si wakati tena wa kulalamika. Lazima mjikomboe wenyewe! Wadaini viongozi wenu Azimio la Arusha kama mlivyowadai katiba mpya.

Wote Wanaokuja kwenu wakidai wanataka kuwakomboa waambieni waje na ahadi ya Azimio la Arusha.

katika mazingira haya, wale wanaofurahia kuvunjwa kwa baraza la mawaziri na kusukwa upya, muda si mrefu wataishia kuweka nyuso zao chini kwa aibu.

Kikwete hawezi kuunda serikali thabiti.

Atapata wapi wa kuwafanya mawaziri? Je, atatoa kwenye chama kilekile – kilichochoka na kinachotuhumiwa kutumia fedha za wizi kuingia madarakani?

Makala hii imeandikwa kwa Msaada wa makala nyingine za Kondo Tutindaga; Paschally Mayega; Joster Mwangulumbi

Advertisements

HALIMA MDEE; PROF. TIBAIJUKA ONYESHA UWEZO KWA VITENDO SI MANENO!

TAARIFA KWA UMMA

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema)

KWA nafasi yangu ya Uwaziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nimefarijika na kauli ya serikali iliyotolewa karibuni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi (Mazingira) Dkt. Terezya Huvisa kwamba nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa, bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992, 1995 na 2004.

Pamoja na kufarijika huko, nimelazimika kutoa taarifa hii kwa umma ili kuwakumbusha wahusika na hususan mawaziri husika sasa wathibitishe uwezo wao na dhamira zao kuwatumikia Watanzania kwa kuwajibika kwa vitendo. Si  kwa maneno.

Nasema haya kwa sababu imekuwa ni kawaida sasa kwa viongozi waandamizi serikalini kuwa ’wazuri’ wa kutoa matamko ya kisiasa, lakini wanapatwa na kigugumizi cha hali ya juu unapotakiwa utekelezaji wa vitendo!

Hii pia inachangiwa na ukweli kwamba vyombo vya dola vinavyopaswa kusimamia utekelezaji wa maagizo mbali mbali ya serikali kutawaliwa na rushwa na uzembe uliokithiri!

Ninayarejea haya kutaka tu kuukumbusha umma wa Watanzania ili wawe makini kufuatilia uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.

Itakumbukwa kwamba kuwa chanzo cha matamshi hayo ya mawaziri, Prof. Tibaijuka na Dkt. Huvisa ni matokea ya ziara iliyofanywa na Waziri wa Ardhi, Jimbo la Kawe, Kinondoni, Dar es salaam.

Ziara ambayo ilishuhudia pasipo kificho, namna ambavyo watu wenye nguvu ya fedha wanadiriki kuharibu mazingira kwa makusudi pasipo kujali athari ambazo zinaweza kutokea sasa na baadae kwa wakazi wa maeneo jirani na Taifa kwa ujumla!

Ninasema kwa makusudi haya kwa kuwa baadhi ya majumba makubwa yaliyojengwa maeneo yasiyoruhusiwa tuliyoyatembelea, yanamilikiwa na viongozi wakubwa Serikalini.

Lakini pia kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kawe kwa kushirikiana na NEMC, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ole Medeye na maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Ardhi na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa nyakati tofauti tulitembelea maeneo yanayotolewa maagizo sasa hivi yakiwa katika hatua ya awali ya ujenzi wa msingi!

Leo ni mengine ni majengo makubwa tayari!

Ndio maana nadiriki kusema yaliyozungumzwa na mawaziri hao sio mapya! Hata kidogo.

Nasisitiza tena, wawajibike kwa vitendo kwa kuchukua hatua ambazo ziko ndani ya uwezo wa serikali. Si maneno.

Nitatoa mifano michache, ambayo kama ingefanyiwa utekelezaji kama amri za serikali zilivyoelekeza hapo awali, ingetosha kuwa fundisho kwa wengine wote ambao wanadhani nguvu yao ya fedha inaweza kuwafanya wawe juu ya sheria na mstakabali wa Watanzania!

1. Mwaka jana 4/1/2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye kumbukumbu namba LD/297571/18 waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhusiana na uvamizi wa kiwanja namba 2019 na 2020  kilichoko Mbezi Kawe.

Katika barua hiyo pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba wizara imefanya ukaguzi katika viwanja Vilivyotajwa hapo juu baada ya kupata malalamiko juu ya uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo.

Barua husika inabainisha kwamba ukaguzi walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika katika eneo husika, ambalo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN) No. 76 ya mwaka 1992 uendelezaji unaofanyika hauruhusiwi.

Kisha ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili unaofanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe.

Barua husika ilisainiwa na bwana Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara.

Tangu barua hiyo iandikwe na kuelekeza hatua zichukuliwe, leo mwaka 1 na miezi 5, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. 

Taarifa za uhakika na ukweli zilizopo, ni kwamba ubomoaji ulikwama mara kadhaa kwa sababu National Environment Management Council (NEMC) pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni walikosa ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni! 


Wasingeweza bomoa pasi na ulinzi! Kuna harufu ya Rushwa.

2. Nyaraka nyingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 toka NEMC kwenda kwa Bwana Frank Mushi. 

Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Bwana Mushi kuvirudisha katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa vifungu 55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004. 

Barua husika inabainisha kwamba timu ya wataalam toka Baraza la Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa ya Kinondoni ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa Kawe Beach.

Timu hiyo ilibaini kwamba mto Ndumbwi, pamoja na bahari ilikuwa inajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020.

Ambapo ndani ya viwanja hivyo lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) , 55(2) (b) , 55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira.

Pia ilibainika kwamba mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira.

Kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza

 i) Timu ya wataalam ilibaini kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilishatoa zuio la ujenzi katika kiwanja husika.

 ii) Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa iliweka zuio la uendelezaji na kutoa amri kwa ’mmiliki’ wa eneo husika kubomoa, lakini mmiliki huyo alipuuza amri hiyo na kuendelea na ujenzi! Taarifa zilizopo Bwana Mushi yupo kama chambo. Nyuma yake kuna kiongozi mkubwa Serikalini. Ukifika wakati mwafaka tutamtaja. 


Hasa iwapo viongozi husika wataendelea ’kuwauzia’ wananchi maneno badala ya vitendo.

 iii) Ilitolewa amri ya Mahakama, tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi asiendelee na ujenzi. Bwana Mushi aliipuuza amri husika na kuendelea na ujenzi.

Baraza la Mazingira lilimwagiza tena, Bwana Mushi:-

 • Kuacha ujenzi mara moja
 • Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro
 • Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri ilitolewa 30/9/2011) awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa maji na bahari na kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya kawaida.
 • Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika hali iliyokuwa awali. Kwa gharama za Bwana Mushi.

Hakuna kitu chochote kilichofanyika! Ujenzi umeendelea, nyumba imekwisha, mto, bahari na mazingira kwa ujumla vimeharibiwa vibaya! Juu ya sheria. Juu ya maslahi ya wananchi wa eneo husika na Watanzania.

3. Nyaraka nyingine ni Taarifa ya Uchunguzi wa Mgogoro wa Ardhi na Mazingira katika eneo la Kawe Beach.

Taarifa hii ilitolewa na Ofisi ya Makamu wa Raisi, Agosti 2010 kufuatia kuundwa kwa kikosi kazi kuchunguza uhalali wa viwanja namba 1040, 1041, 2000, 2002 na 1071.

Chanzo cha mgogoro husika ni kubuniwa kwa viwanja vya nyongeza kando kando ya Mto Mbezi katika eneo linaloelekea baharini, hali inayopelekea maji ya mto kutuama na kuharibu mazingira na makazi ya wananchi walio jirani na eneo hilo!

Kamati ilifanya kazi yake na kutoa mapendekezo mazuri yenye lengo la kuokoa mazingira! Tangu mwaka 2010 hadi leo hakuna kilichofanyika!

Kitu kinachoshangaza na kusikitisha ni UJASIRI na WEPESI wa kutoa matamko, kuunda kamati au vikosi kazi, lakini vikosi kazi baada ya kufanya kazi yake, linapokuja suala la utekelezaji wahusika, wakiwemo mawaziri wanapatwa na vigugumizi.

Haijulikani wanakopata pia ujasiri wa kutoa visingizio wakati sheria ziko wazi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60 ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa ziwa.

Halikadhalika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 (Sura 113) Fungu 7 (1) (d) inabainisha kwamba eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari linatakiwa kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa.

Pale inapotokea kuwa masharti ya Sheria moja yanapingana na Masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu mambo yanayohusu usimamizi wa Mazingira, Sheria ya Mazingira ndiyo hutumika, kwa mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura 191 ya mwaka 2004.

Ndio maana nasisitiza! Hatuna haja ya kutoa matamko! Walio na mamlaka, waliokabidhiwa dhamana, sasa tufanye kazi kwa vitendo!

Haitoshi tu kutamka maneno makali ya kisiasa, wananchi wanataka kuona uwezo wenu dhahiri kwenye kuchukua hatua, tena zilizoko ndani ya uwezo wenu kisheria.

Si vinginevyo.

Nadhani ni wakati muafaka sasa kwa Waziri wa Ardhi , wakati akijiandaa kuvunja majumba yote yaliyojengwa ufukweni kufanya tathmini yale aliyokwisha yatolea matamko huko nyuma, yamefanikiwa kwa kiwango kipi!

Namkumbusha hili sambamba na ahadi zake kwa Watanzania za kurudisha viwanja vya wazi vyote vilivyovamiwa.

Zoezi ambalo limekuwa likienda kwa kusuasua sana!

Awaambie amefikia wapi au anakwamishwa na nini kilicho juu ya sheria na maslahi ya umma wa Watanzania.

Tunataka viongozi wa serikali waelewe kuwa Watanzania wamechoka na maneno na ahadi za kila siku ambazo hawaoni utekelezaji.

Wanataka ’kuuziwa’ matendo si maneno!


Halima Mdee (MB)

Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MASIKINI MIZENGO PINDA, BAADA YA KUNUSURIKA KWA WABUNGE UPEPO WA KUMG’OA BADO WAMWANDAMA.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

• Khamis Mgeja, ataka naye ang’atuke kama mawaziri wenzake.

• Yusuf Makamba, alimlipua kwamba hana mawasiliano mazuri na serikali.

• Kingunge asema kwa kutokujiamini kwake ndiyo sababu ya wananchi kupoteza imani kwa CCM na serikali yake.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anaendelea kuandamwa na jinamizi la kutaka kumng’oa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), mjini Dodoma ikiwa ni ndani ya wiki 3 tu toka kunusurika kung’olewa na Bungeni.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilicho malizika Jumanne Mei 15, 2012 mjini Dodoma zilidai kuwa baadhi ya wajumbe wa NEC waliibua hoja ya kumtaka Pinda apime uzito wa tuhuma zinazo mwandama Bungeni na achukue hatua za kuwajibika.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa Pinda kwa kuibua hoja ya kumtaka naye ang’atuke.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mgeja akichangia ajenda ya hali ya kisiasa ndani ya chama hicho, alisema haoni sababu ya Waziri Mkuu kutowajibika wakati mawaziri wake wamewajibika, tena wengine si kwa makosa yao bali ya uzembe uliosababishwa na watendaji wao.

Mgeja alisema Pinda anapaswa kuwajibika kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali ulioainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Huku akiungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa NEC kwa kupiga makofi, mwenyekiti huyo alisema CCM inapakwa matope kwa makosa ya viongozi wa serikali kutowajibika na kusisitiza kuwa Pinda anapaswa kupima uzito wa hoja kwani ndiye kiranja wa mawaziri waliong’olewa kwa tuhuma za ufisadi.

Alihoji kuwa kama mawaziri wanane wameng’olewa kutokana na ripoti ya CAG na shinikizo la wabunge wakiwemo wa CCM kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Pinda, Waziri Mkuu huyo hana uhalali wa kubaki madarakani akaendelea kuaminika.

Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya kikao hicho, alisema Mgeja alitoa mfano wa ufisadi wa mamilioni ya fedha unaofanywa na watendaji katika wilaya za mkoa wake kupitia vocha ya pembejeo kwamba ni wa kutisha, na alishatoa taarifa kwa waziri mkuu ambaye hakuzifanyia kazi hadi sasa.

Hoja hiyo iliungwa mkono Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba, ambaye alimlipua Waziri Mkuu Pinda kwamba hana mawasiliano mazuri na serikali.

Alisema haridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo kwani ni rahisi kumpata Raisi kuliko waziri mkuu, jambo ambalo alisema halileti tija kwa serikali.

Mjumbe mwingine aliyekosoa utendaji wa Pinda ni mkongwe Kingunge ngombale Mwiru ambaye alimtaka mtendaji huyo kufanya kazi kwa kujiamini ili kurejesha imani ya wananchi kwa CCM iliyoanza kupoteza Mwelekeo

Habari zinasema kuwa wakati Pinda akishambuliwa na kutakiwa kujiuzulu, Mwenyekiti wa CCM Taifa, RaisiKikwete, na Pinda mwenyewe, hawakujibu chochote.

NCHEMBA AJIPA KAZI YA AFISA HABARI WA BOT NA KUMJIBU ZITTO KATIKA KILE KILICHODAIWA “BENKI KUU HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA”.

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimesikitishwa na kushangazwa na taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari hivi leo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.

Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera. Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi.

Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.

Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa.

Lakini vilevile, ningetegemea kwamba, kama ameamua kusambaza taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki Kuu.

Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni, kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.

Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo.

Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.

Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.

Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe.

Hili limenishangaza kwasababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni.

Huu ni utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.

Pili, ningetegemea pia Mhe. Zitto awe anafahamu kwamba kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board).

Huko nyuma, Kamati hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika Benki Kuu vipunguzwe.

Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati hii inayopitisha taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili. Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu.

Mara ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari, ambayo imekwishasambazwa.

Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka.

Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo.

Mimi ndicho nilichofanya, na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja kama alivyodai Mhe ZITTO.

Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia tarehe 11 May 2012).

Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.

Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.

Imetolewa na:

Mwigulu Lameck Nchemba (MB)

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa

Dodoma 13 Mei 2012

ZITTO KABWE; BENKI KUU, HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA?

Mweshimiwa Zito Zuberi Kabwe

Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo.

Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin).

Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya Kimataifa na Deni la Taifa.

Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu Jumapili Mei 13, 2012 utakuta Taarifa hizi.

Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba.

Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita nyuma.

Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?

Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu.

Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.

Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!

Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.

Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.

Taarifa zinafichwa.

Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu.

Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi.

Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa macho.


Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali.

Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!

Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita.

Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu.

Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi.

Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu. 


Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.

Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka.

Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili).

Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.


Imetolewa na:

Zitto Zuberi Kabwe (MB)

Waziri wa fedha Kivuri, Mwenyekiti Kamati ya bunge ya Mashirika ya Umma

13 Mei 2012

WANAHARAKATI WAPENDEKEZA RIPOTI YA CAG ITUMIKE KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA, WANASHERIA WAPINGA.

 • Diana Mwiru; “kila kitu kiko wazi tunachunguza nini tena”
 • Amina Uddy asema “Uwajibikaji wa viongozi umepungua, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi”.
 • Wanasheria wasema ripoti ya CAG haitoshi kuwafikisha wahusika mahakamani Uchunguzi wa TAKUKURU na DCI hauepukiki.

WANAHARAKATI nchini wamepinga   mpango wa Ikulu wa kutaka kuwapo na uchunguzi wa watendaji katika wizara na taasisi nyingine za umma wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma kwa kigezo kwamba ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inatosha kuwafikisha mahakamani.

Kauli hiyo imekuja baada ya Alhamisi Mei 10, 2012 Ikulu kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watendaji hao kwa kile walichoeleza ni hatua za awali kabla ya kufungua kesi mahakamani.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia katika mtandao wa Maendeleo na Jinsia (GDSS), Diana Mwiru alisema kwa sasa hakuna haja ya kufanya uchunguzi kwa kuwa ripoti ya CAG na zile za kamati tatu za bunge zinaonyesha wazi namna wahusika walivyohusika katika tuhuma hizo.

“Tuhuma zinazowahusu mawaziri zinatokana na wao kushindwa kuwajibika na kulisababishia hasara taifa, … ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali (CAG) na ripoti za kamati tatu za bunge zote  ziko wazi na wote tumeona hasara iliyotokea ,hoja yangu ni kwamba tunachunguza nini tena? alihoji Mwiru na kuongeza:

“Kinachotakiwa kwa sasa ni wahusika kufikisha mahakamani kujibu tuhuma, unafanyika uchunguzi mwingine wa nini, hawa wanatufanya sisi hatujui kitu, kazi ya Takukuru ni kuchunguza rushwa swali ni je tuhuma hizo ni za rushwa? alihoji Mwiru.

Mwiru alisisitiza kuwa chunguzi zilizofanywa zinatosha na sasa watanzania wanataka kuona watuhumiwa wakifikishwa kwenye muhimili mwingine unao tafsiri sheria (Mahakama) ili kuona haki inatendeka.

Mawaziri waliondolewa katika nafasi zao walitajwa katika ripoti ya CAG, na pia ripoti za kamati za kudumu za bunge zilizowasilishwa kwenye vikao vya bunge lilifanyika hivi karibuni mkoani Dodoma.

Kamati hizo ni ile ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (POAC) ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira  Mwenyekiti wake , James Lembeli zilionyesha namna mawaziri walivyoshindwa kuwajibika na kusababishia taifa hasara kubwa.

Ripoti za kamati hizo Bungeni ziliibua tuhuma za upotevu wa fedha huku zikiwataja baadhi ya mawaziri kushindwa kuwajibika hali iliyomsukuma Bunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe kuitisha hoja ya kukusanya saini za kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Amina Uddy mwanaharakati toka ForDIA alisema, hali ya uwajibikaji nchini imeshuka kwa kiwango kikubwa hali inayowafanya viongozi washindwe kujali na kusimamia rasilimali za umma.

Alisema ripoti zimebainisha matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma kwenye  Mashirika ya Umma,  serikali za mitaa na serikali kuu ambapo kuna upotevu mkubwa wa mali za umma ikiwamo suala la ulipaji mishahara hewa.

“Uwajibikaji wa viongozi umepungua, maadili yameporomoka na hii inathibitika wanapotaja mali wakati wa kuingia kwenye nyazifa zao lakini wanapotoka hawataji mali zao, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi” alisema Uddi.

Uddi alitaja sababu zinazochangia hilo kuwa ni pamoja na vitendo vya kuporomoka kwa maadili ya viongozi na mhimili wa Dola kuingilia mamlaka ya utendaji wa  mihili mingine ya mahakama na bunge.

Baadhi ya wanasheria walio ongea na M2S wamesema Kimsingi TAKUKURU (au vyombo vingine vinavyohusika na maswala ya uchunguzi wa jinai  kwa  mfano polisi au mwendesha mashtaka mkuu wa serikali) wanao uwezo wa kufanyia kazi taarifa hizi kwa maana ya kuanza uchunguzi. 

Hilo halina shaka. Sababu ni kuwa vyombo hivi havibanwi na sheria eti kusubiri “taarifa maalumu” ndipo waanze uchunguzi wa makosa. Wanaweza kufanyia kazi hata tetesi, au hata mere “suspicion” tu. 

Na ndio maana hata kazi zake ni pamoja na “kuzuia” rushwa na makosa ya jinai-yaani kuchukua tahadhari kabla hayajatokea. 

Kwa mfano kifungu cha 7 cha sheria ya takukuru ambayo inasema wazi kuwa kazi ya takukuru ni “investigate any alleged or suspected offence under this Act”.

Kama kuzuia walishidwa, basi wanapokua na shaka “suspicion” kwa kosa ambalo tayari limeshatendeka wanalo bado jukumu la kuchunguza mazingira yake ili kujiridhisha kwamba ni kweli au la.

Kwa hiyo, hizo taarifa za bunge na CAG ni sababu tosha ya vyombo hivyo kuanza huo uchunguzi (trigger of investigation). 

Sio lazima wachunguze mawaziri tu bali kila mtu anayehusishwa na kutenda hayo makosa ya rushwa, awe waziri au wafanyakazi wa chini yake, wanapaswa kuchunguzwa, na kama kuna ukweli katika hizo tuhuma wapelekwa mahakamani.

Cha msingi ni watanzania wajue kuwa hizo report pekee haziwezi kutosha kushinda kesi. Hizo ni, kama nilivyosema, triggers tu za uchunguzi. Kisheria zinaweza hata kuwa pungufu ya asilimia 50 ya ushaidi unaotakiwa. 

Ila zinaweza kutoa mwanga wa nani wachunguzwe, tuhuma gani, wapi wachunguze na watumie mbinu gani. 

Kama unakumbuka swala la Richmond na Rada watu walipiga sana kelele kwamba kwanini kesi hazikupelekwa mahakamani. 

Kunaweza kuwa siasa kweli zilitumika kuzima, lakini pia ikawa sio kweli. Mahakama zinafuata sheria na sio siasa.

Mamlaka yenye uwezo wa kufungua kesi za jinai dhidi ya watuhumiwa wa makosa hayo mahakamani ni mkurugenzi wa makosa ya jinai (DPP), ama mamlaka nyingine ambayo kisheria imepewa hiyo haadhi na DPP, au na sheria. Hii inaweza kuwa kwa mfano takukuru, polis n.k.

Tuchukue mfano wa takukuru. Takukuru yenyewe (on its own) haina mamlaka ya kufungua kesi mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika hadi iruhusiwe na DPP. 

Baada uchunguzi inapeleka kabrasha la uchunguzi huo kwa DPP ambaye akijiridhisha kwamba kweli kuna kesi inayoweza kufikia viwango vya kisheria kupelekwa mahakamani na ushindi ukapatikana (na sisitiza: viwango vya kisheria, sio kelele za kisiasa) basi anaruhusu kesi ifunguliwe.

Hili ni tatizo kwa sheria yetu ya rushwa hapa Tanzania. Nchi nyingine zimetoa mamlaka kwa taasisi zao za kupambana na rushwa kuweza kufungua kesi moja kwa moja bila kusubiri ruhusa ya DPP. Yaani, PCCB na DPP wangetakiwa wawe mamlaka mbili huru, zisizo tegemeana kwa namna yoyote. 

Bahati mbaya sisi bado tuko nyuma sana. Na katika hili tuko nyuma kiutendaji ukilinganisha na ule Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa dhidi ya Rushwa ambao unahitaji vyombo kama takukuru kuwa independent kwa kila Nyanja.

MADIWANI WA TARIME WAMKATAA MTEULE WA JK KUWA MKUU WA WILAYA.

 • Wadai yeye ndiyo chanzo cha kuzorota mahusiano kati ya mgodi wa Barrick na wananchi.

  Wagoma kufanya vikao vyovyote katika halmashauri ikiwa Rais Kikwete hatamwondoa.

 • TAMISEMI wasema hawana mamlaka ya kinidhamu ya kumuwajibisha mkuu wa wilaya.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Alhamisi Mei 10, 2012 kwa kauli moja waligoma kuendelea na mkutano wa Baraza la Madiwani wakipinga hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuteua tena John Henjewele kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Henjewele ni miongoni mwa wakuu wa wilaya 63 waliobaki katika uteuzi mpya wa wakuu wa wilaya. Kati ya wakuu 70 wapya, saba ni wana habari.

Madiwani hao ambao walikutana katika kikao cha kawaida kilichoitishwa kujadili mbali na mambo mengine taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), walisema hawako tayari kuendelea na vikao vyovyote katika halmashauri ikiwa Rais Kikwete hatamwondoa mkuu huyo wa wilaya kwa madai kwamba amekuwa akiendesha utawala wake kwa ubabe.

Bila kujali itikadi za vyama vyao, madiwani hao 41 walisema watachukua hatua ya haraka kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa kumtaka awasilishe ujumbe wake kwa Rais Kikwete wakiomba kuondolewa haraka wilayani hapo kwa Henjewele.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amos Sagara aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuvunjika kikao hicho kuwa alilalizimika kuahirisha kikao hicho kutokana na jazba za wazi zilizoonyeshwa na wawakilishi hao wa wananchi dhidi ya mkuu wa wilaya.

“Sasa katika mazingira kama hayo wameniomba nimuite mkuu wa mkoa ambaye walisema wanataka kuongea naye kabla ya kuendelea na kikao chochote nami sikuwa na pingamizi kwa kuwa walidai hawamtaki mkuu wa wilaya,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia uzito wa suala hilo atachukua hatua za haraka kuwasiliana na mkuu wa mkoa ili kumkutanisha na madiwani kwa kuwa kisheria hawana mamlaka ya kumuwajibisha DC kutokana na kuwa mteule wa Rais.

Miongoni mwa tuhuma zilizoainishwa na madiwani hao baada ya kugomea kikao hicho ni pamoja na kuingilia utendaji wa kazi ngazi za serikali ya vijiji wakidai amekuwa akiwaondoa wenyeviti wa serikali ya vijiji na kukaimisha watu wake bila kufanyika uchaguzi.

Diwani wa Kata ya Turwa, Charles Ndesi, alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa chanzo cha kuzorota mahusiano kati ya wamiliki wa mgodi wa Barrick na wakazi wanaozunguka viunga vyake katika mji wa Nyamongo huku wananchi wakizidi kuwa maskini na uvamizi wa mara kwa mara katika mgodi huo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Fidelis Lumato alisema wao kama taasisi ya Wizara ya TAMISEMI hawana mamlaka ya kinidhamu ya kumuwajibisha mkuu wa wilaya bali aliye na uwezo huo ni rais peke yake.

MAWAZIRI WAPYA WAAPISHWA; WASEMA YALIYO MOYONI MWAO

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wake Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu Kiongozi, wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wateule baada ya kuapishwa rasmi Ikulu Dar es Salaam

•    Wahaidi kukabiliana na changamoto.
•    Makamba asema kazi yake ya kwanza ni kupitia upya garama za simu hapa nchini.
•    Dk. Mgimwa asema hakuna kitakacho shindikana, yeye kujikita zaidi na mfumko wa bei.

Rais Jakaya Kikwete amewaapisha mawaziri wapya pamoja na manaibu wake wakuu Jumatatu Mei 07, 2012 ikulu jijini Dar es Salaam.

Awali rais alifanya uteuzi huo kwa kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza lake kwa kuingiza sura 13 mpya huku mawaziri na naibu mawaziri nane wakitupwa nje ya baraza hilo.

Katika mabadiliko hayo, amewapandisha naibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha mawaziri nane na naibu mawaziri sita, huku mawaziri na naibu mawaziri 22 wakibaki katika wizara zao za awali.

Mawaziri wapya watio apishwa na Wizara zao kwenye mabano ni Mbunge wa Handeni,  Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa  Sospeter Muhongo (Nishati na Madini).

Manaibu Mawaziri wapya ni Mbunge wa Rufiji, Dk Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (Nishati na Madini-  Nishati), Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Mbunge wa Mvomero, Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Wengine ni Mbunge wa Makete, Dk Binilith Mahenge (Maji), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Maselle (Nishati na Madini ), Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (Katiba na Sheria) na wabunge wa kuteuliwa, Janet Mbene na Saada Mkuya Salum ambao wote wamekuwa Manaibu Waziri wa Fedha.

Naibu Mawaziri waliopandishwa na kuwa mawaziri kamili ni Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).

Baada ya kuapishwa baadhi ya mawaziri walinukuliwa wakisema malengo yao pamoja na vipaumbele vyao katika nafasi zao hizo mpya.

Dk Mgimwa
Waziri mpya wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa, alinukuliwa akisema kuapishwa kwake ni jambo la heshima hivyo ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania.

Alipoulizwa jinsi atakavyo kabiliana na changamoto ndani ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na tuhuma zilizomng ‘oa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Mustapha Mkulo, Dk Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Kalenga alisema kabla ya kufanya lolote ni lazima kujiridhisha.

“Bungeni tulikuwa tunazungumza mengi kuhusu wizara hii lakini niseme kwamba ni lazima ufanye tathmini na ukishajua hali halisi ya tatizo ndio unaweza kuzungumza suluhisho la tatizo husika ni nini, hakuna kisichowezekana,” alinukuliwa Dk Mgimwa

Makamba
Kwa upande wake Naibu mpya wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema moja ya mambo ya kufanya katika wizara hiyo ni kutazama upya gharama za mitandao ya simu.

“Wizara hii inagusa maisha ya kila siku ya Mtanzania hivyo kuna ulazima wa kutizama gharama za mitandao ya simu ili iendane na maisha halisi ya mtanzania” alisema Makamba.

Akizungumzia masuala ya sayansi, Makamba alisema kuwa kuna ulazima wa kutizama upya msingi wa elimu ya sayansi kuanzia shule ya msingi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma somo hilo.

Pia, aligusia mikakati iliyowekwa awali ya asilimia moja ya pato la taifa kuingizwa katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali na kwamba umefikia wakati wa suala hilo kuanza kutekelezwa kikamilifu.

“Tunatakiwa kuondoa urasimu wa matumizi ya teknolojia, hakuna haja ya watumishi wa Serikali na wananchi kupanga foleni kwa ajili ya kuchukua fomu, huu ni wakati wa fomu kujazwa katika mitandao tu,” alisema Makamba.

Hata hivyo, Makamba alisema kuwa mambo mengi anayoyaona na kuyazungumza hata bungeni yameshaanza kufanyiwa kazi na wizara hiyo.

Rashid

Naibu Waziri mpya wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Suleiman Rashid alisema kuwa kipaumbele katika wizara hiyo ni kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi, tena kwa ubora mkubwa.


“Huduma ya afya inatakiwa kuwafikia watu wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mgonjwa anasafirishwa eneo moja mpaka jingine kwa usalama” alisema Dk Rashid.


Rashid ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji alisema kuwa wizara inatakiwa kushughulikia sera na kutengeneza mipango mizuri ili watumishi wake wafanye kazi katika mazingira bora kwa faida yao na Watanzania wote.


Tizeba
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa alisema kwa kuwa ni msaidizi wa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, atahakikisha kila jambo analofanya bosi wake linakwenda sawa.


“Namshuruku sana Rais Kikwete, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa kuwa wao ndio waliopendekeza mimi kuteuliwa kuwa waziri, nitatumia elimu yangu na uzoefu katika Serikali katika utendaji wangu wa kazi” alisema Dk Tizeba.


Mahenge
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Dk Binilith Mahenge ambaye ni Mbunge wa Makete, alisema kuwa atazungumza zaidi mara baada ya kuapishwa.

 

Masele
Akizungumzia kuapishwa kwake Masele alisema kwanza atapambana kudhibiti mali ya umma, kuhakikisha udhibiti wa madini na kupata thamani halisi ya kile kinachozalishwa.


Pia alisema atashughulikia matatizo ya wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakinyonywa ili waweze kupata haki zao stahiki na kuinua uchumi wao.


“Niwahakikishie Watanzania kwamba nimepewa nafasi kubwa na nitafanya kazi kwa uadilifu, “alisema Masele.


Aliongeza kuwa; “Tutahakikisha tunazipitia sheria na kuhakikisha wamiliki wa migodi wanawasaidia wananchi na kila sehemu ulipo mgodi tutashughulikia ili wananchi na serikali vyote vinufaike.”

Alisema kuna watu wanapotosha kuhusu elimu yake, lakini ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) ambako alihitimu mwaka 2004.

Pia amewahi kufanya kazi katika benki kabla ya kupata nafasi ya kuwa Meneja Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Tigo.

KATIKA DHANA YA UWAJIBIKAJI WATENDAJI KWENYE WIZARA ZENYE SHUTUMA WAJIUZURU.

Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaapisha mawaziri wateule Jumatatu Mei 7, 2012. kushika nafasi hizo mpya, Tayari baadhi ya wabunge wamewataka mawaziri hao wasifanye sherehe kwa kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa; zikiwemo zilizosababisha mabadiliko yanayowapa nafasi.

Tunaunga mkono japo tungependa mabadiriko zaidi lakini sura mpaya ndani ya baraza hilo la mawaziri linatufanya turejeshe imani kidogo na serikali yetu. 

Kwa upande wetu tunafahamu kuwa moja ya sababu ya matokeo hayo ni uwepo wa watendaji wa Serikali ambao wamechangia kwa sehemu kubwa kuzembea katika nafasi zao na kumlazimu Rais Kikwete kuwawajibisha mawaziri kisiasa.

Watendaji hao wanajua kuwa baada ya mawaziri kuwajibika, wanafuata wao ili iwe fundisho kuwa utendaji mbovu utakaosababisha waziri, au Serikali kuwajibika kisiasa.

Mazingira hayo ya uwepo wa watendaji wanaosubiri kuwajibishwa, yanaweza kuwa kikwazo cha kazi kwa mawaziri hawa hasa kama atalazimika kufanya kazi kwa karibu na mtendaji anayetuhumiwa au ambaye anajijua anahusika na uzembe uliosababisha Serikali kuwajibika kisiasa.

Lakini tunashauri uzembe wa mtendaji ambaye anafuata nyayo za mawaziri waliowajibika kisiasa, usitumike kuwakwaza wateule wapya kwa namna yoyote kwa kuwa vikwazo vya namna hiyo, mwisho wake vina athari katika mustakabali wa maisha ya Watanzania.

Tunashauri kwamba lingekuwa jambo la uungwana na zaidi uzalendo kwa watendaji hao kuwa mstari wa mbele kuonesha kujuta na kuwasaidia wateule wapya kutekeleza majukumu yao wakati wakisubiri adhabu yao.

Katika kujenga dhana ya uwajibikaji katika jamii ya Watanzania, haitakuwa vibaya kwa mtendaji ambaye amehusika moja kwa moja na uzembe na anajijua kwa hilo, kujiuzulu ili kujijengea heshima katika mustakabali wa maisha yake katika utumishi wa umma.

Inajulikana kuwa kujiuzulu si rahisi, ni vigumu na wakati fulani inahitaji kujikana. Lakini ni jambo lililo wazi kwamba wengi waliojiuzulu na kukiri makosa, walijijengea heshima kulikowaliosubiri kuondolewa kwa kuwa mwanadamu kukosea kaumbiwa.


MHE. ZITTO KABWE: MAWAZIRI, HAKUNA SHEREHE, NENDENI MKAWAJIBIKE!

Mweshimiwa Zito Zuberi Kabwe

Juhudi za kurejesha misingi ya uwajibikaji katika utumishi wa umma zimeanza kuzaa matunda Baada ya Rais kutekeleza shinikizo la Bunge la kuwafukuza kazi baadhi ya Mawaziri ambao Wizara zao zimetuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma, rushwa na utendaji mbovu.

Mawaziri 6 wamefukuzwa kazi baada ya kugoma kujiuzuru wao wenyewe, manaibu waziri 2 wamefujuzwa pia.

Ndugu George Mkuchika alitakiwa kujiuzuru, akajiuzulu lakini Rais amemrudisha kwenye Baraza kama Waziri wa Utawala Bora. Yeye nampongeza kwani hakuwa na makuu ya kuanza kujitetea kama wengine. atakuwa ametoa funzo kwa wenzake.

Kwa kawaida wateule hufanya sherehe kwa kuteuliwa kwao. Nitawashangaa watakaofanya sherehe safari hii kwani hakuna cha kufurahia.

Nitawashangaa watakaokwenda kuapa na Maua kwa furaha kwani furaha itakuwa ya muda mfupi tu.

Mkutano wa Bunge wa Bajeti ni mwezi ujao tu na wateule wote watakuwa kikaangoni. Too short honeymoon.

Hakuna cha kusherekea kwa sababu nchi ina changamoto nyingi sana.

Changamoto ya kuzalisha umeme wa kutosha na kuusambaza kwa wananchi wengi, changamoto ya kukuza uchumi wa vijijini na kukuza uzalishaji viwandani ili kutengeneza ajira kwa vijana, changamoto ya kuongeza mapato ya Utalii kutoka katika hifadhi zetu na kuvutia watalii zaidi katika nchi yetu.


Nimewapigia simu wateule wengi na kuwaambia, siwapi pongezi Bali nawatakia kazi njema. Nawatakia uwajibikaji mwema. Uwajibikaji ndio msingi wa kupambana na rushwa, uvivu na uzembe.

Kwa Waziri wa Fedha, ambaye mimi ni Waziri Kivuli wake (Kama  Kiongozi wa Upinzani Bungeni hataniwajibisha pia), namwambia uteuzi wake ni changamoto kubwa sana katika maisha yake.

Hivi sasa eneo lenye Bajeti kubwa kuliko zote nchini ni huduma kwa Deni la Taifa (services to national debt). Lazima kuangalia upya Deni la Taifa. Hivi sasa Deni la Taifa ukijumlisha na Dhamana za Serikali (government guarantees) limefikia tshs 22trn mpaka Desemba 2011.

Nimewahi kutaka ukaguzi Maalumu katika ‘account’ ya Deni la Taifa. Linarejea wigo huu. Tunalipa takribani 1.9trn tshs kwa mwaka kuhudumia Deni la Taifa. Zaidi ya Bajeti ya miumbombinu, Afya, Maji, Umeme nk.

Mfumuko wa Bei, misamaha ya kodi na kodi zinazozuia watanzania kujiajiri ni changamoto kubwa sana Wizara ya Fedha lazima ihangaike nayo.

Usimamizi wa Mashirika ya Umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na hasa usimamizi wa Hisa za Serikali katika kampuni binafsi ni masuala yanayohitaji masuluhisho sasa na sio baadaye.

Kwa Mwalimu wangu Dkt. Mwakyembe, utakumbukwa kwa Jambo moja tu. RELI. “make our railway system work”. Hutakuwa na ‘legacy’ nyingine isipokuwa reli maana Bandari bila Reli ni sawa na Bure.

Tunatumia zaidi ya tshs 300bn kwa mwaka kukarabati barabara wakati tunahitaji tshs 200bn kukarabati Reli iweze kusafirisha mzigo kwenda Bandarini na kutoka Bandarini.

Ndiyo maana nasema hakuna Jambo la kusherehekea maana wajibu mliopewa na Rais ni mtihani mkubwa kwenu katika kulitumikia Taifa letu.

Msipowajibika, mtakumbwa na fagio la chuma!

Mkisha kula kiapo, kimbienikKazini. Nothing to celebrate. hit the ground running.

Imetolewa na:

ZZK

Dar-es-Salaam, Jumamosi Mei 5 2012.

NINI KILICHOMO KWENYE RIPOTI YA CAG .

Ludovick Utouh

SIKU chache baada ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kubariki uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kulisuka upya Baraza la Mawaziri kwa kuwaondoa waliotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu wamekataa kuchukua hatua hiyo.

Kwa zaidi ya wiki mbili sasa, kumekuwa na shinikizo la kutaka mawaziri wanane wajiuzulu nyadhifa zao kutokana na wizara zao kutajwa na CAG kwamba zimehusika na ufisadi huku wengine wakitajwa moja kwa moja kufanya uamuzi wenye maslahi binafsi.

Wengi wetu tumekuwa tukifwatilia mnyukano huo ndani na nje ya bungeni baina ya wabunge na Serikali pamoja na mawaziri hao kuhusu ubadhilifu wa fedha za walipa kodi.

Katika ripoti hiyo ambayo wengi awajaiona na M2S kupata nakala zake imeonyesha mapungufu mengi kama mishahara hewa yenye thamani ya sh583.2 milioni. Vilevile matumizi ambayo serikali imeyafanya bila kuidhinishwa na bunge.

Baadhi ya Matumizi ambayo hayakuidhinishwa ni matumizi ya Sh21.63 bilioni zilizotumika kuendesha mfuko wa kukwamua wananchi kiuchumi maarufu kama ‘mabilioni ya JK’.

Vile vile ripoti hiyo imeonyesha udanganyifu na ukwepaji kodi uliyoisababishia hasara Serikali ya sh15.4 Bilioni na Dola 2.6 milioni za Marekani, kiasi ambacho ni kikubwa.

Kutokana na taarifa hiyo Wananchi na baadhi ya wabunge wametaka wahusika wawajibishwe, zifwatazo ni baadhi ya tuhuma zinazo wakabili mawaziri pamoja na baadhi ya manaibu wao.

 

Mustapha Mkulo – Waziri wa Fedha na Uchumi.

Shutuma zinazo mkabili Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ni kuuzwa kwa kiwanja cha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) kwa kampuni ya Mohamedi Enterprises Tanzania Ltd kinyume cha taratibu.

Ukaguzi  wa CAG unadai kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha zilihusika moja kwa moja katika uuzwaji wa Kiwanja Na.10 kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere kilichouzwa kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises Tanzania Ltd bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). 

Vilevile, CAG anadai kuwepo kwa utata katika hati ya madai ya Sh 2.4 bilioni kutoka katika Kampuni ya DRTC kama gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya kuingia kwenye Kiwanja Na.192 kando ya Barabara ya Nyerere. 

Ripoti hiyo vilevile inadai mapungufu yalionekana pia kwenye uuzwaji wa jengo la Kampuni ya Tanzania Motors (TMC) lililopo kiwanja Na.24 kilichopo kando ya Barabara ya Ali Hassani Mwinyi.  

Pia, Menejimenti ya CHC haikuwa makini kwenye uuzaji wa kiwanja Na. 33 kilichopo katika eneo la viwanda la Chang’ombe kwa Kampuni ya Maungu Seed.

 

Dk Hadji Mponda – Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.

Kadhia inayo ikabili wizara hii ya Afya na Ustawi wa Jamii ni shutuma juu ya Bohari ya Madawa (MSD) ambapo ukaguzi maalumu wa MSD uliofanyika ulibaini kuwapo tofauti ya Sh 658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokelewa na kuripotiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwenda MSD.

Pia ripoti imeonyesha kulikuwa na kiasi cha Sh100 milioni kilichopokelewa na MSD kutoka Wizara ya Afya na kikatumiwa na MSD bila kuwepo na mchanganuo wa matumizi.

Katika ripoti hiyo kuna kiasi cha Sh 4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununua dawa na vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh 4.344 bilioni tu ndicho kilichopokelewa na MSD ikiacha Sh 196 milioni bila kuwepo na ushahidi wa kupokelewa na MSD kutoka Wizara ya Afya.

Madai mengine ni kuwa, baadhi ya vifaa vinavyotolewa na MSD vimekuwa havina viwango vinavyostahili, kwa mfano vifaa vya kupima shinikizo la damu na machela za kubebea wagonjwa zilizotolewa kwa mganga mmoja wa wilaya (DMO), viliharibika kabla ya muda uliokusudiwa. 

Utata mwingine ni juu ya matumizi ya jumla ya Sh1.10 bilioni kwa ajili maonyesho ya Nane nane, fedha ambazo hazikuwamo kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge.

 

Omar Nundu – Waziri wa Uchukuzi.

Tatizo katika wizara hii ni tuhuma dhidi ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam. 

CAG katika ukaguzi wake inadai Shirika la Ndege Tanzania limekuwa likijiendesha bila Bodi ya Wakurugenzi kwa muda mrefu jambo ambalo limesababisha kudorora kwa shughuli za shirika hilo.  

Sakata jingine ni la mkataba kati ya ATCL na Shirika la Ndege la Afrika Kusini uliovunjika kutokana na sababu mbalimbali za kiutendaji. 

Baada ya kuvunjika kwa mkataba huo Septemba 2006, Shirika la Ndege Tanzania lilisaini mkataba mwingine wa makubaliano na Kampuni ya China Sonangol International Holdings Limited. 

Kampuni hii ilileta ndege mbili chakavu ambazo zilikuwa zikitumiwa na shirika jingine kinyume na makubaliano. Ndege zilizoletwa ni aina ya Bombardier Dash 8-Q400s ambazo zilikuwa zimekwishatumiwa na mashirika mengine ya ndege na nyingine aina ya Airbus A320 ambayo ilikuwa na umri wa miaka 10 hadi kufikia mwaka, 2007.

Januari 2009 ndege aina ya Airbus A320 ilipaswa ipelekwe kwenye matengenezo makubwa yanayofanyika kila baada ya miaka minne hadi mitano. 

Julai, 2009 ndege hii ilirudishwa kwa mwenyewe. Hata hivyo, wakati akijibu majumuisho ya hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge pamoja na mawaziri, Mwenyekiti Kamati ya Bunge za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe alisema taarifa aliyonayo ni kwamba kampuni hiyo iliyoikodishia ndege ATCL imepewa zabuni ya kuendesha Bandari ya Mtwara.  

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Sakata jingine ni usimamizi mbaya wa Mkataba wa Ujenzi Katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).  

TPA iliingia katika mkataba na kampuni ya AF MULT-Con LTD kujenga nyumba ya makazi ya msimamizi mkuu wa Bandari ya Tanga kwa gharama ya Sh 500 milioni. 

Taratibu za zabuni na maridhiano ya mkataba huo yalihakikiwa na hapakuwa na dosari. Hata hivyo, ilibainika udhaifu wa usimamizi na kutotekelezwa kwa masharti ya mkataba yalisababisha mradi kushindwa kuendelea licha ya Mkandarasi kulipwa asilimia 20 ya bei ya mkataba yaani Sh100 milioni.

Katika sakata jingine lililosababishwa na usitishwaji wa mkataba ulipelekea malipo batili. wakati wa ukaguzi wa taarifa ya fedha za TPA za mwaka wa fedha 2010/2011 ilibainika  kwamba mamlaka hiyo iliingia katika mkataba wa ujenzi wa ukuta wa uzio katika Bandari ya Mtwara na Kampuni ya Chibeshi Contruction.

Mkataba huo ambao uligharimu shirika Jumla ya Sh 679.8 milioni ulisainiwa Aprili, 14 2009 na kukubaliana kuwa utakamilika baada ya wiki 26 kuanzia tarehe ya kusaini mkataba.  

Hata hivyo, kabla ya mkandarasi kuanza kazi, mamlaka iliamua kuvunja mkataba kwa madai kuwa hapakuwa na mgao wa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo.  

Usimamizi na uamuzi wa kuvunja mkataba uliifanya Mamlaka kulipishwa faini ya Sh92.5 milioni na mkandarasi. Kanuni ya Na. 46 (5) na (6) GN 97 ya mwaka 2005 inaeleza bayana kwamba, gharama za mahitaji ya manunuzi ni lazima zikadiriwe na kulinganishwa na uwezekano wa upatikanaji wa fedha ili kuweka vipaumbele katika manunuzi muhimu.

Kanuni ambayo haikuzingatiwa na uongozi wa mamlaka na hivyo kutoa nafasi kwa mkandarasi kulipwa tozo ya Sh92.5 milioni.

Katika sakata lingine ripoti inasema kuwa kutolipwa kwa tozo ya fidia za uvunjifu wa mikataba kati ya TPA na Kampuni ya WIA ni sawa na mamlaka kuingia  mkataba wa kubuni au kusimika.

Mkataba huu ulikuwa kwa ajili ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai 2010 hadi Oktoba 2010, lakini haukuweza kukamilika kwa muda wa kipindi cha mkataba hivyo kupelekea mamlaka kumuongezea mkandarasi muda hadi Februari, 2011.

Licha ya mkandarasi kuongezwa muda, hakuweza kukamilisha kazi aliyopewa.  Kutokana na upungufu huo mkandarasi alitakiwa ailipe mamlaka fidia ya ucheleweshaji ya asilimia 10 ya bei ya mkataba Dola za Kimarekani elfu 95.3 fedha ambazo hazikulipwa kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana.

 

Ezekiel Maige – Waziri wa Maliasili na Utalii

Kadhia inayoikabili wizara hii ni baada ya ripoti ya CAG kuonyesha kuwa Wizara ilipoteza Sh874,853,564 baada ya kufanya maamuzi ya upendeleo ya kutoa kiwango cha chini cha mrabaha kwa mazao ya misitu. 

Ukaguzi wa hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA) umeonyesha kuwa Shirika liliingia mkataba tata na kampuni ya CATS Tanzania LTD unaohusiana na matengenezo ya kawaida, ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine katika mkataba wa jumla ya dola za Kimarekani milioni moja. 

 

Dk Cyril Chami 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Chami anakabiliwa na kashfa ya ukaguzi wa magari ya wakala wa Shirika la Vwango Tanzania (TBS).

Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ilipendekeza kuwajibishwa kwa afisa masuhuli wa wizara ya viwanda na biashara kwa kuisababishia serikali hasara ya dola  18,343,540 za Marekani ambazo ni karibu Sh30 bilioni.  

Kamati ya Bunge pia inasema kuwa Kamapuni wakala wa kukagua magari wa TBS zilizopo nje ya nchi ni feki na kwamba wamiliki wake ni watanzania waliop nchini. 

Alisema pia imegundua kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kukodi majengo ya wizara na kusisitiza kuwa wizara moja inaweza kulipa kodi ya Sh485 milioni. 


William Ngeleja 

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ataachia ngazi baada ya CAG kubaini kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa mwaka mmoja wa fedha linafanya manunuzi yenye thamani kati ya Sh300 bilioni hadi Sh600 bilioni.

Kwa mwaka wa fedha 2009/2010, Tanesco  ililitumia 1.8 bilioni ukilinganisha na Sh65 Milioni zilizokuwa zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati mojawapo katika kituo cha bwawa la Mtera.    

Pia Ngeleja anatuhumiwa Wizara ya Nishati na Madini chini yake iliingia mikataba ya madini isiyokuwa na tija  kwa taifa.

  

George Mkuchika  

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika naye ataachia ngazi  baada ya ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kubaini mtandao mkubwa wa wezi wa mali za umma.

KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM KUTOA SULUHISHO LA TUHUMA ZA MAWAZIRI LEO?

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete

 • Nape hagoma kusema ajenda za kikao
 • Mawaziri wanao tuhumiwa nao wanena

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameitisha kikao cha ghafla cha Kamati Kuu ya chama hicho kujadili pamoja na mambo mengine, hali ya siasa nchini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, amethibitisha habari hii na kueleza kuwa kikao hicho kitafanyika Aprili 27, 2012 Ikulu Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Ingawa Nape alisema hawezi kutaja ajenda za kikao hicho kwa kuwa ni siri, habari kutoka baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, zilisema kwavyovyote vile ajenda ya shinikizo la mawaziri hao kujiuzulu ni moja wapo.

Nape alishindwa kuthibitisha au kukanusha taarifa kwamba kikao hicho kitajadili hatima ya mawaziri hao wanaotakiwa kujiuzulu badala yake akasema, “Ni kweli kesho tuna Kamati Kuu Dar es Salaam, lakini agenda za kikao hicho haziwezi kuwekwa ‘public’ ujue hivyo tu inatosha,” alisema Nape.

Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ni Kepteni George Mkuchika (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula  na Ushirika), Mhandisi Omar Nundu (Uchukuzi) pamoja na  Mkulo na Nyalandu.

Shinikizo la kutaka mawaziri nane wajiuzulu liliibuka katika Mkutano wa Saba wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, baada ya ripoti hiyo ya CAG kuonyesha tuhuma nzito za ufisadi katika wizara hizo huku baadhi ya mawaziri wakionekana kuhusika moja kwa moja na maamuzi waliyofanya.

Mkulo ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu, kutokana na kashfa ya kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL),  alisema  hawezi kuzungumzia suala la kujiuzulu kwa sababu hajui kosa lake wala madai ya wabunge dhidi yake.

Alipoulizwa kama yuko tayari kujiuzulu kuhusiana na kashfa zinazoikabili wizara yake, Mkulo alijibu, ‘ hapa, no comment,” akiwa na maana kwamba hana cha kuzungumza.

“Kwanza sifahamu tuhuma zilizotolewa na wabunge kwa sababu sikuwepo, mimi nilikuwa safari,” alisema.

Kwa upande wake Nyalandu alisema kuwa, mpaka sasa haelewi kwanini ameingizwa kwenye kashfa hiyo kwa sababu katika ripoti ya CAG, hakutajwa na wenyeviti wa kamati mbalimbali za kudumu za Bunge.

“Sielewi kwanini nimeingizwa kwenye kashfa hii kwa sababu katika ripoti ya CAG sikuwemo. Ripoti ya Mwenyekiti wa Kamati ya POAC na PAC simo pia, lakini nilishangaa nilipoanza kusikia jina langu,” alifafanua Nyalandu.

Tayari Nyalandu alitoa waraka unaonyesha msimamo tofauti na wa bosi wake, Dk Chami kuhusu kashfa zinazowakabili ambazo ni tuhuma alizonazo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekelege anayedaiwa kuanzisha kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi hususani, Hong Kong na Singapore.

Wakati Nyalandu akishauri Ekelege asimamishwe kazi ili apishe uchunguzi wa CAG na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu arudishwe kazini, waziri wake (Chami) alisema kuwa Ekelege ni mteule wa rais, hivyo hawezi kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka amwondoe wakati hakuna taarifa yoyote inayoonyesha tuhuma zake.

Kwa upande wake,  Dk Mponda anayekabiliwa na kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD)pamoja na upotefu wa pesa za wizara hiyo amesema leo atatoa ufafanuzi wa kitugani kilitokea.

Waziri  Maige juzi aliamua kueleza baadhi ya tuhuma zinazomkabili ikiwamo umiliki wa nyumba aliyodaiwa kuinunua kwa Dola 700,000 za Marekani, akisema nyumba hiyo aliinunua kwa dola 410,000 na siyo dola 700,000 kama ilivyoelezwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Mazingira, James Lembeli alipinga kauli hiyo akisema taarifa alizonazo zinaonyesha Maige alinunua nyumba hiyo kwa fedha taslimu dola 700,000.

Kashfa nyingine inayomkabili Maige ni ile iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira huku ikitaka awajibishwe kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kampuni ambazo hazina sifa na kusafitishwa nje kwa wanyama wakiwamo twiga na tembo kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Maige alisema  hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa baina ya viongozi mbalimbali na kwamba habari mbaya dhidi yake zinalenga kumchafua kutokana na kuwa mkali katika utendaji wake wa kazi na kuongeza, kuna chuki kutokana na kwamba aliwahi kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wizarani kwake  jambo ambalo limewaudhi baadhi yao.