Uchaguzi wa Arumeru Mashariki umekwisha na matokeo yake yametangazwa na hivyo wananchi wa Arumeru Mashariki tayari wamejipatia mwakilishi wao. Huku baadhi ya viongozi wa serikali na vyama pendwa wakisema demokrasia imechukuwa mkondo wake.

Mengi yalisemwa kabla na baada ya uchaguzi huo kufanyika. Mimi binafsi nilitoa tahadhari kabla ya uchaguzi kuhusu matokeo ya kushangaza yatakayotokea Arumeru Mashariki katika makala yangu iliyotolewa na Tazama katika toleo na. 491. Iliyokuwa na kichwa cha habari “Jimbo la watu makini wasiokubali kuburuzwa.”

Kimsingi Arumeru Mashariki wamechagua mabadiliko. Na si kwamba CHADEMA ni chama bora na makini sana, la hasha, Watanzania wengi, zaidi vijana wanaonyesha kukichukia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Miongoni mwao ni Wana-CCM wenyewe. Kiukweli, mvuto wa Chama Cha Mapinduzi kwa Watanzania na hususan vijana unazidi kupungua. Hayo yamethibitishwa na wengi akiwemo Mwenyekiti wake.

Makala hii haitawapendeza wengi wetu, na kwa bahati mbaya kalamu yangu haiko kwa ajili ya kuwapendeza watu fulani fulani hivyo niko radhi nitengeneze uadui kwa kusema ukweli ili tukinusuru chama hiki kikongwe kabisa hapa nchini. Wanachama wenye mapenzi ya ukweli na CCM wamejikunyata huku wakitafuta nani aliyesababisha anguko lao.

Viongozi na wapenzi wa CCM wakiwa bado wanaweweseka na matokeo ya Arumeru yawapasa kujua lililotokea na kusababisha anguko lao ili safari hii wajiwinde sawia na uchaguzi mdogo unaotegemewa kufanyika katika jiji la Arusha ambapo kuna nafasi sita za udiwani na moja ya mbunge.

Lengo letu si kumyooshea kidole mtu mmoja mmoja, bali ni kutafuta kasoro zilizo jitokeza hasa ndani ya kambi ya CCM pale Arumeru Mashariki. Ningependa tuungane pamoja katika utafiti tuliofanya kutoka katika vyanzo anuai vya kuaminika ndani ya serikali na katika duru za CCM

Kinachotokea sasa ndani ya chama ni ‘ Witch hunting’- kutafutana uchawi. Bila shaka, kuna maswali yanayo paswa kuulizwa. Moja kubwa ni hili; Je CCM ilistahili kushindwa? Na msukumo wa swali hilo ni katika kumtafuta mchawi na kukitenganisha chama na uzembe wa makusudi au bahati mbaya uliopelekea katika ‘Anguko la Arumeru’.

Ni ukweli usiyopingika CCM waliingia kwenye ushindani wa Arumeru Mashariki wakiwa wachovu. Tunashindwa kujua tatizo lilikuwa nini lakini ikilinganishwa na Igunga kampeni za Arumeru zilifanyika kwa mazoea tu.Hakukuwa na mikakati ya ushindi, hotuba hazikuandaliwa vizuri, haukufanyika utafiti na kupata majibu ya matatizo ya watu wa eneo husika.

Kwa hesabu rahisi Chadema walionekana ni wenyeji zaidi pale Arumeru Mashariki na kufanikiwa kufanya mikutano 128 huku CCM wakionekana wageni na kutokujuwa matatizo ya wananchi wa maeneo hayo walijikongoja kwa idadi ya mikutano 73 tu. Je kwa maantiki hii walitarajia ushindi?

Ilionekana wazi kwamba CCM waliingia katika kampeni za ubunge huku kukiwa na kambi ambazo hazikuvunjwa baada ya Uchaguzi wa kumchagua mgombea ndani ya chama. Hawakuwa wamoja na hata hoja zao ziliweza kuonyesha tofauti kubwa za kiahiba. Hata wanahabari waliopenda kulifunika hilo hawakupata hoja ya kutetea mpasuko huo.

Mitaani walijinasibu waziwazi, hata baada ya matokeo kutoka wapo wanachama wa chama cha mgombea aliyeshindwa walishindwa kuficha furaha zao. Hapo tunajiuliza, je walikuwa wanafanya kampeni kwa moyo mmoja au walikuja kumharibia mgombea wao?.

Kwa aliyefuatilia kampeni hizi tangu uteuzi ndani ya vyama, hawezi kuwa na wasiwasi kwamba makundi yamedhoofisha ushindi wa chama hicho na kuongeza nguvu za wapinzani wao. Tayari tulianza kuambiwa uteuzi wa mgombea husika ulikuwa ushindi wa kambi mojawapo.

Pamoja na kutokuwa na umoja vilevile napata wasiwasi na vigezo vilivyo tumika kuchagua timu ya kampeni ya Arumeru. Hili liko wazi kutokana na wengi walio chaguliwa ni wale wale waliokuwa wanampinga mgombea huyo bila kujificha.

Kwa mara ya kwanza katika harakati za kuomba kura kwenye chaguzi ndogo, tuliona muungano wa mashaka wa makundi hasimu ndani ya CCM, yaani wale wanaojiita makamanda wa kupambana dhidi ya ufisadi kwa upande mmoja na wale ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa ufisadi kwa upande mwingine.

Hata kama hatua hii ilikuwa kwa nia njema ukweli ni kwamba tofati hizo zilionekana wazi wazi na ziliwagawa wana CCM. Ndio maana Kuonekana kwa Sitta Kirumba, Ole Sendeka na Mpambanaji kijana Nape Nnauye Arumeru Mashariki, Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela kata ya Kiwira kuliwafanya wananchi waiadhibu CCM kwa kutumia masanduku ya kura.

Kwa tafsiri rahisi katika chaguzi hizi ndogo hususan Arumeru Mashariki, CCM waliendeleza siasa za Umamluki ambazo hukibomoa chama chako mwenyewe na siyo cha mpinzani wako.

Hakuna aliyeshangazwa na kitendo cha Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alipoamua kuporomosha matusi dhidi ya viongozi wa Chadema badala ya kujenga hoja za kumuombea kura mgombea wake. Haingii akilini kuwa mweshimiwa huyo hakujua madhara ya uamuzi wake alioufanya tena katika wiki ya mwisho ya kampeni hizo.

Je? kitu gani kilimsukuma Mheshimiwa huyo kufanya hayo? Majibu ni mengi ila ukweli kwamba haikuwa kwa faida kwa chama chake ni jambo lisilo na ubishi. Kumejitokeza fikra mpya kwasasa kutokana na utetezi unaofanywa na viongozi wazito wazito ndani ya chama kuwa huenda mheshimiwa huyu alitumwa na viongozi hao.

Swali lingine wenye chama chao wanapaswa kujiuliza ni hakukuwa na mtu yeyote ndani ya chama aliyekuwa na uthubutu wa kuyakemea matendo hayo yasiyokuwa ya kistaarabu? Inavyo onekana Mheshimiwa huyu aliendesha siasa zake za mwituni huku akiungwa mkono na Katibu Mkuu wa chama chake Wilson Mukama na wengine kwa faida wanazo zijuwa wenyewe.

Mfano wa uadilifu uliopaswa kufanyika ni kama ule alioufanya Mheshimiwa Waziri Mkuu Mstaafu Edwadi Lowassa alipotoa sharti la kutokuruhusiwa kwa matusi katika mikutano ambayo yeye angemnadi mgombea wa CCM. Na ndiyo maana katika mkutano wa Kikatiti Livingstone Lusinde hakuonekana.

Tatizo jingine lililoikabili timu ya kampeni lilikuwa kushindwa kujenga hoja zenye ushawishi kwa wananchi. CCM wanapaswa kujifunza kwamba hoja haiwezi kusimama kama haigusi maslahi ya wapiga kura. Kusimama na kumshutumu mtu tena asiye mgombea kwamba si wa familia ya Nyerere ni kiwango cha juu cha kushindwa kujipambanua kwa fikra mpya.

Lilipotokea mara ya kwanza tulijua kuwa aliyesema aliteleza. Lakini kuendelea kwa makada wa CCM Stephen Wassira, Nchemba na Livingstone Lusinde kumshambulia Vincent na kudai pia kuwa watu wa Arumeru hawahitaji taarifa za Nyerere ili kuondokana na shida zao za kila siku zilionyesha wazi kutokujipanga kwa timu hiyo ya kampeni.

Shutuma au makombora mengi yaliyo rushwa na CCM yalishindwa kufanya yale yaliyokusudiwa na  kuambulia utetezi kutoka vyombo na asasi nyingine likiwemo kanisa Katoliki na Familia ya Baba wa Taifa kulizidisha imani na kukipa nguvu chama cha Chadema na kuwafanya CCM kuonekana wanafanya siasa za Giliba.

Kuna hoja nyingine ambayo inadaiwa kuwa mgombea wa CCM, Sioi hakupewa fedha za kutosha na chama chake kwa ajili ya kampeni kwani hadi zinamalizika, CCM ilikuwa imetoa fedha kiduchu tu tofauti na ilivyofanya kwa wagombea wengine kwenye chaguzi ndogo ambako chama hicho hubeba gharama zote.

“Mpaka usiku wa tarehe 30/03/2012, chama kilikuwa kimetoa milioni 60 pekee kwa kampeni nzima, fedha ambazo hazikutosha hata kulipa mawakala 327 na wale wa akiba ambao kila mmoja alitakiwa kulipwa Sh30,000. Yaani kama vile chama kilijitenga na kampeni za Sioi,” alisema na kulalamika kiongozi mmoja aliyeongoza kampeni za mgombea huyo.

Taharifa za ndani zinasema gharama za kampeni za mgombea huyo wa CCM zilikuwa zaidi Sh200 milioni ambazo zilitokana na michango binafsi ya wanafamilia na marafiki zake.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alipoulizwa kuhusu madai hayo, alikataa kusema lolote akisisitiza kwamba hayo ni mambo ya ndani ya chama yanayostahili kuzungumzwa na kujadiliwa ndani ya vikao.

Pamoja na kunyimwa kwa fedha za kutosha pia inaelezwa kuwa CCM ilimtenga mgombea wake na kumuachia afanye kila kitu mwenyewe. Mfano dhahiri wa kutengwa kwa mgombea huyo ni siku ya kupiga kura ambako hakuna kiongozi yeyote aliyehangaika kuzunguka vituoni kukagua.

Hali ilikuwa mbaya zaidi ilipofika wakati wa kukusanya masanduku ya kura na matokeo kutoka vituoni kabla majumuisho yaliyofanyika katika ofisi ya mji mdogo wa USA-River, ambako hakukuwa na kiongozi yeyote aliyejitokeza kusimamia wala kushuhudia majumuisho hayo.

“Huwezi kuamini kuwa hakukuwa na kiongozi wala mwakilishi yeyote wa CCM kwenye chumba cha majumuisho ya kura hadi ilipofika Saa 7:00 usiku, ndipo mgombea mwenyewe alipoamua kwenda kushuhudia na kusimamia kura zake,” alisema mjumbe mmoja wa CCM ambaye ni kiongozi wa ngazi ya mkoa.

Sioi alifika eneo hilo akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa vijana wa CCM (UVCCM), Benno Malisa pamoja na makada wengine watatu ambao hata hivyo, waliondoka baada ya dakika 40 na kumuacha mgombea huyo peke yake.

Sioi Sumari, alibaki ukumbini hapo akiwa ameketi viti vya nyuma hadi alipoondoka ukumbini Saa 10:30 alfajiri, huku mwenzake, Joshua Nassari wa Chadema waliyekuwa wakichuana vikali akiwa ameketi mbele akiwa amezungukwa na kundi kubwa la viongozi wa kitaifa na mawakala wake.

Jambo la mwisho la kujiuliza kwanini katibu mwenezi Mpambanaji kijana Nape Nnauye baada ya kusambaz habari za kushindwa kwa chama chake kwenye mitandao ya kijamii kabla hata ya matokeo kutangazwa alikubali haraka haraka kushindwa kwa chama chake bila hata kuwasilihana na mgombea wake? haraka ilikuwa ya nini? je kwa kauli yake ilikuwa ni kumzima mgombea wake asiweze kukata rufaa au kupinga matokeo?

Timu ya Kampeni ya Chama Cha Mapinduzi Arumeru Mashariki ilikuwa kama Jogoo ambalo hudhani kila siku Jua huchomoza ili lisikilize linavyowika. Kwa mantiki hiyo kama CCM wanataka kujifunza, basi wajifunze kwamba siasa za makundi, mtandao na maslahi yasiyo ya kitaifa hayawezi kukipa ushindi.